************************
Na. Prisca Maduhu, DODOMA
Shule ya Sekondari Itega inatekeleza mradi wa ujenzi wa darasa na ofisi ndogo ya walimu kwa lengo la kupunguza msongamano wa wanafunzi darasani na kuwapokea kidato cha kwanza mwaka 2023 ili kuimarisha ufanisi wa kazi na kupunguza msongamano wa walimu katika ofisi moja.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa shule ya sekondari Itega, Mwl. Briton Bwatota wakati akisimamia mradi wa ujenzi wa darasa moja na ofisi ndogo ya walimu katika shule ya sekondari Itega iliyopo Kata ya Nkuhungu katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Mwl. Bwatota alisema kuwa shule ya sekondari ya Itega ilipokea kiasi cha shilingi 20,000,000 katika utekelezaji wa mradi huo. Aliongeza kuwa kiasi hicho cha fedha kilipokelewa tarehe 1-10-2022 na kuanza ujenzi rasmi tarehe 10-10-2022.
Aliendelea kusema kuwa, fedha hizi zitatumika katika ujenzi wa darasa moja, ofisi ndogo ya walimu, ununuzi wa vifaa vya ujenzi pia ununuzi wa samani za darasani ambazo ni viti na meza.
Mkuu huyo wa shule alisema kwamba kiasi cha shilingi 6,434,000 kimetumika na kubakiwa na shilingi 13,566,000 kwenye akaunti. Ujenzi huo umefikia katika hatua ya kuweka lenta ambapo ni sawa na asilimia 63% ya ujenzi huo, aliongeza.
Alisema kuwa aliunda kamati tano kwa ajili ya kufanikisha utekelezaji wa mradi huo. Alizitaja kamati hizo kuwa ni kamati ya mapokezi, kamati ya ujenzi, kamati ya manunuzi, kamati ya utekelezaji mradi na “tender bord”. Pia alisema kuwa walitoa matangazo ya kutafuta fundi ujenzi, ambapo tangazo hili walilitoa katika ofisi ya kata na kubandika matangazo, na baadae kuwapata mafundi na kuwafanyia usaili ili kumpata fundi ambaye amekidhi vigezo.
“Mradi huu ni msaada mkubwa katika shule yetu, utasadia kupunguza msongamano wa wanafunzi darasani na kwa walimu utasadia kuongeza uwajibikaji,” alisema Mwl. Bwatota.
Ikumbukwe kuwa shule ya sekondari Itega ilianzishwa mwaka 2007, mpaka sasa ina wanafunzi 771 ambapo wasichana ni 323 na wavulana ni 448.