Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Angeline Mabula akiwasalimia wananchi wa kijiji cha Kibengu katika halmashauri ya Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa wakati Kamati ya Mawaziri Nane inayoshughulikia migogoro ya Matumizi ya Ardhi katika vijiji 975 ilipotembelea kijiji hicho kilichopo hifadhi ya shamba la Sao hill Oktoba 26, 2022
Sehemu ya wananchi wa kijiji cha Kibengu katika halmashauri ya wilaya ya Iringa waliojitokeza kwenye mkutano wa hadhara na Kamati ya Mawaziri Nane wa Wizara za Kisekta inayoshughulikia migogoro ya matumizi ya ardhi katika vijiji 975.
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Khamis Hamza Chilo.
Naibu Waziri Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega
Naibu Waziri wa Maji Meryprisca Mahundi
Naibu Waziri wa Kilimo Anthony Peter Mavunde
Naibu Waziri OR-TAMISEMI David Silinde
Naibu Waziri Maliasili na Utalii Mary Masanja
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Angeline Mabula (waliosimama mbele katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Mawaziri wa Wizara za Kisekta wanaoshughulikia migogoro ya matumizi ya ardhi katika vijiji 975. Wa pili kulia ni Mkuu wa mkoa wa Iringa Halima Dendegu
(PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)
……………………………….
Na Munir Shemweta, IRINGA
Kaya 255 za vijiji vitatu vya Igeleke, Usokami na Kibengu vilivyopo halmasauri ya wilaya ya Mufindi mkoani Iringa zitaondolewa eneo la hifadhi ya Shamba la Sao Hill.
Uamuzi huo umetangazwa na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula Oktoba 26, 2022 wakati Kamati ya Mawaziri Nane wa Wizara za Kisekta inayoshughulikia migogoro ya matumizi ya ardhi katika vijiji 975 ilipotembelea na kukutana na wananchi wa kijiji cha Kibengu kilichopo wilaya ya Mufindi mkoani Iringa.
Dkt Mabula alisema uamuzi unaofanywa kuhusiana na eneo hilo una nia njema kwa mustakabali wa taifa na vizazi vijavyo kwa kuwa kaya hizo zimekuwa zikifanya shughuli za kibinadamu ndani ya hifadhi ikiwemo kilimo cha mazao ya kudumu na mazao ya msimu na kuharibu mazingira.
Alitaja idadi ya kaya kwa kila kijiji kuwa, ni kaya 4 za kijiji cha Igeleke kinachohusisha vitongoji vya Kihesa, Mdodi, Lwombogole na Igangilonga. Kaya nyingine ni 97 za kijiji cha Usokami zilizoko vitongoji vya Kidete, Msega, Mgwao, Ilamba, Nyamifwa na Uhwana pamoja na kaya 154 za kijiji cha Kibengu ambazo zote zitatakiwa kuondoka.
“Hiyo ni takwimu za kaya zinazoenda kuathirika na siyo kuhama eneo moja kwenda lingine lakini kwa utaratibu maalum na hakuna atakaye kuja kusema ondokeni leo” alisema Dkt Mabula.
“Mhe Samia amesema hamtaondoka bure na uthamini itafanyika kwa yoyote aliyetimiza masharti na kwa kuwa kijiji kimeandikishwa maana yake mmekidhi vigezo vya kulipwa, na kila mlichowekeza katika eneo husika hakuna atakayedhurika”
Baadhi ya mapendekezo ya wataalamu kuhusiana kaya zinazotakiwa kuondoka eneo la hifadhi ya msitu wa Sao Hill mkoani Iringa ni pamoja na kuwekwa ukomo kwa wananchi kuondoa miti ndani ya hifadhi sambamba na Hifadhi kutoa notsi ya kisheria kwa wananchi kuondoa miti yao kabla ya tarehe ya ukomo.
Mkoa wa Iringa unahusisha vijiji/mitaa 15 yenye migogoro ya matumizi ya ardhi ambapo vijiji hivyo vimeainishwa katika sehemu kuu sita kulingana na aina ya mgogoro na uamuzi uliotolewa na Baraza la Mawaziri.
Manaibu Mawaziri wa Wizara za Kisekta waliopo katika ziara hiyo kila mmoja alielezea umuhimu wa sekta yake katika kulinda na kuimarisha rasilimali za nchi kupitia sekta ya ardhi.
Khamis Hamza Chilo mbali na kupongeza upandaji miti ya biashara wilayani Mufindi alishauri wananchi kupanda miti ya kudumu ili kurithisha vizazi vijavyo.
‘’Nasema haya kwa sababu Tanzania kwa sasa inalia na kuathirika kwa mabadiliko ya tabia nchi na tuchukue tahadhari na kujitahidi kwa kutunza mazingira na kupanda miti ili mwisho wa siku tusilete athari kwa viumbe hai’’. Alisema Chillo
Kwa upande wake Naibu Waziri Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega alielezea umuhimu wa kuwa na ng’ombe wa maziwa na kushauri wananchi wa Mufindi kujitahidi kila mmoja kuwa na angalau ng’ombe wawili na kusisitiza kuwa, Wizara yake iko katika jitihada za kuimarisha shamba lake sehemu ya Sao hill.
Davida Silinde, Naibu Waziri OR-TAMISEMI alisema ofisi yake kuanzia sasa mchakato wa kusajili vijjji utafanyika kwa ushirikiano na wizara nyingine za kisekta ili kuepuka migogoro ya ardhi inayojitokeza mara kwa mara.