Mkurugezi mkuu wa TEMDO, Profesa Frederick Kahimba akionyesha moja ya teknolojia zinazotengenezwa na taasisi hiyo hapa nchini.
Mkuu wa kitengo cha mawasiliano na masoko (TEMDO)Dk Sigisbert Mmasi akionyesha teknolojia mojawapo ya kiteketezi cha taka za hospitali kwa wananchi waliotembelea banda hilo katika maonesho ya Sido jijini Arusha.
………………………………..
Julieth Laizer ,Arusha.
Arusha.Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya uhandisi na usanifu wa mitambo Tanzania (TEMDO),Frederick Kahimba amesema kuwa, katika kuhakikisha wananchi wanaondokana na gharama kubwa ya kuagiza teknolojia nje ya nchi wameendelea kubuni teknolojia mbalimbali kwa lengo la kukuza uchumi wa viwanda ambapo sasa hivi wamekuja na teknolojia mbadala ya kukausha zao la mihogo kwa muda mfupi na kuendelea kubakia na virutubisho ambavyo vinatakiwa .
Aidha wakulima wa zao la mihogo mara nyingi wamekuwa wakipata hasara kubwa kutokana na zao hilo kuharibika hasa kwenye mchakato wa ukaushaji kutokana na kutokuwa na mashine ya kukaushia zao hilo.
Ameyasema hayo leo jijini Arusha ,wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye maonesho ya SIDO yaliyofanyika jijini Arusha wakati akitambulisha mtambo huo mpya kwa wananchi waliotembelea banda hilo kujionea teknolojia mbalimbali ikiwemo hiyo ya mihogo .
“Mtambo huu wa mihogo usanifu wake ulianza miaka miwili iliyopita ambapo mtambo huo umekamilika mwaka huu wa fedha ,ambapo awali wakulima wa zao la mihogo walikuwa wanalazimika kutumia siku nyingi katika kukausha mihogo hali ambayo wakati mwingine inaharibika na inawapotezea muda mrefu “amesema Kahimba.
Amesema kuwa, uwepo wa teknolojia hiyo utaweza kuwarahisishia kazi wakulima wakati wa usindikaji kwani watalazimika kutumia siku moja pekee tofauti na hapo awali ambapo walikuwa wanatumia siku zaidi ya 10 huku wakitumia nishati kama jua kama chanzo cha ukaushaji.
“Kwa kutumia teknolojia hiyo mkulima ataweza kuvuna mhogo wake na akaukausha siku hiyo hiyo na akaweza kufungasha unga katika vifungashio tayari kwa matumizi ya nyumbani kwa kweli uwepo wa teknolojia hii ni mkombozi tosha wa wakulima wa mihogo na naomba sana wakulima wachangamkie hiyo fursa.”amesema Kahimba.
Aidha ametoa wito kwa wananchi na taasisi mbalimbali kupenda kutumia bidhaa za ndani zinazotengenezwa hapa nchini kwani zinapunguza gharama kubwa ya kuagiza nje na endapo vikiharibika vinatengenezewa hapa hapa nchini.
Kwa upande wake Mkuu wa kitengo cha mawasiliano na masoko TEMDO, Dk Sigisbert Mmasi amesema kuwa,amesema kuwa kitendo cha taasisi hiyo kuja na teknolojia hiyo kimekuwa mkombozi mkubwa kwa wakulima kutokana na adha kubwa na gharama walizokuwa wakipata pindi wakivuna mazao yao.
Aidha amewataka wajasirimali ambao ni wamiliki wa viwanda kuhakikisha wanatumia uwepo wa taasisi hiyo hasa katika uvumbuzi wa mashine na teknolojia mpya ambazo zote zinalenga kuinua uchumi wa Taifa.
Amesema kuwa,huwa wanawawezesha wadau wa viwanda kwa kuwapa elimu na namna sahihi ya kutumia teknolojia hizo kwa ajili ya matumizi mbalimbali ndani ya viwanda na hatimaye elimu hiyo kuwafikia idadi kubwa ya watu ambao wamekuwa wakinufaika.
“Lengo letu ni kuona kuwa sekta hasa ya viwanda inakuwa na mapinduzi makubwa kwa kuwa tuna uwezo mkubwa sana wa kutengeneza vitu ambavyo hapo awali vilikuwa vinatengenezwa nje ya nchi ambapo hivi sasa tunazalisha na kubuni kwa umahiri mkubwa ,hivyo ni fursa sasa kwa watanzania na wamiliki wa viwanda kutumia taasisi hii ili kwa pamoja tujenge uchumi wa viwanda.”amesema Dk Mmasi.