Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja(Mb) akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Kibengu Wilaya ya Mufindi Mkoani Iringa kuhusu kushirikiana kudhibiti moto katika mashamba ya miti,wakati wa ziara ya Kamati ya Mawaziri wa Kisekta katika Shamba la Miti Sao hill.
Baadhi ya wananchi wakimsikiliza Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja(Mb) (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao wakati wa ziara ya Kamati ya Mawaziri wa Kisekta katika Shamba la Miti Sao hill kwenye Kijiji cha Kibengu Wilaya ya Mufindi Mkoani Iringa.
Kamati ya Mawaziri wa Kisekta ikiongozwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Dkt. Angeline Mabula (Mb) katika kikao na Mkuu wa Mkoa wa Iringa ilipofanya ziara mkoani humo.
Kamati ya Mawaziri wa Kisekta ikiongozwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Dkt. Angeline Mabula (Mb) (katikati) katika picha ya pamoja ilipotembelea Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa kwa ajili ya ziara ya kutatua migogoro ya ardhi mkoani humo.
……………………….
NAIBU Waziri wa Maliasili na Utalii,Mhe.Mary Masanja(Mb) amewataka wananchi Mkoani Iringa kushirikiana katika kudhibiti matukio ya moto yanayojitokeza kwenye mashamba ya miti binafsi na ya Serikali.
Ameyasema hayo leo katika Kijiji cha Kibengu Wilaya ya Mufindi Mkoani Iringa wakati wa ziara ya Kamati ya Mawaziri wa Kisekta katika Shamba la Miti Saohill.
“Niwaombe sana kila mtu awe mlinzi wa mwenzake, kama unaandaa shamba hakikisha unaangalia upepo unaelekea wapi ndipo uchome” amesisitiza.
Amewaomba wananchi kuwasiliana na viongozi wa mashamba inapofikia wakati wa kuandaa mashamba yao ili waweze kuwa karibu kudhibiti moto ambao unaweza ukajitokeza .
Amefafanua kuwa mashamba ya miti yamekuwa msaada mkubwa kwa wananchi kwa kutoa ajira akitolea mfano wa Shamba la Miti Sao Hill ambalo limekuwa likitoa ajira zaidi ya 4000 kwa wananchi.
Amesema Shamba hilo pia limekuwa likisaidia katika huduma mbalimbali kwa jamii kama kusaidia ujenzi wa madarasa,zahanati, vituo vya afya pamoja na ujenzi wa shule
Aidha, shamba hilo pia huzalisha Miche ya miti ipatayo milioni 7 kila mwaka ambayo hupandwa kwenye maeneo yaliyovunwa , huwagawia wananchi na Taasisi mbalimbali binafsi.
Ziara ya Kamati ya Mawaziri wa Kisekta inaendelea mkoani Njombe Oktoba 25, 2022