Katibu Tawala Mkoa wa Rukwa Bw. Rashid Mchatta akifungua kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa leo mjini Sumbawanga ambapo amewataka watumishi hao kuzingatia mifumo ya utendaji serikalini ili kuleta tija zaidi.
Sehemu ya wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi ya Mkuu wa Rukwa wakifuatilia agenda za kikao hicho leo mjini Sumbawanga.
Bi. Lucy Mjema ambaye ni Mwakilishi wa TUGHE mkoa wa Rukwa akitoa salamu za chama hicho leo kwenye kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Sekretariati ya mkoa wa Rukwa.
************************
Na. OMM Rukwa
Katibu Tawala Mkoa wa Rukwa Rashid Mchatta amewataka watumishi wa umma kutumika mifumo rasmi ya uendeshaji shughuli za serikali ikiwemo mabaraza ya wafanyakazi kuongeza tija mahala pa kazi.
Akifungua kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa leo (Jumanne Oktoba 25, 2022) mjini Sumbawanga, Mchatta amesema ni wajibu wao kuzingatia taratibu za utumishi wa umma.
“Tutumie mifumo rasmi ikiwemo mabaraza ya wafanyakazi kutoa mchango wa kuboresha utendaji kazi wa serikali. Kila mmoja wenu anapaswa kujua dira na mwelekeo wa taasisi ili kufikia malengo yaliyokusudiwa”alisisitiza Mchatta.
Katika kikao hicho, Mchatta amewataka watumishi hao kuelewa dira ya mkoa huo ili wachangie kuleta maendeleo kwa ustawi wa wananchi ambapo amesisitiza pia kudumisha nidhamu mahala pa kazi.
Mchatta aliongeza kusema “nidhamu, maadili na utaratibu wa kufuata sheria, taratibu na kanuni kwa watumishi wa umma ni jambo muhimu ili kuleta ustawi wa taasisi”
Kuhusu utekelezaji wa miradi ya maendeleo Mchatta ametoa wito kwa wakuu wa idara na vitengo pamoja na Makatibu Tawala Wilaya kuendelea kufanya usimamizi wa karibu na kuhakikisha ifikapo Mwisho wa mwaka huu wa fedha ziwe zimetumika kwa mujibu wa sheria.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali Kuu na Afya (TUGHE) Mkoa wa Rukwa Lucy Mjema alipongeza Sekretariati ya mkoa wa Rukwa kwa kufanya vikao vya baraza ya wafanyakazi kwa muda uliopangwa hatua inayosaidia kuongeza tija mahala pa kazi na kupunguza changamoto za watumishi.
Kikao hicho cha Baraza la Wafanyakazi kimehudhuriwa na wajumbe toka wilaya za Kalambo, Nkasi na Sumbawanga ambapo kilijadili na kupokea taarifa kuhusu bajeti ya mwaka 2022/23 .