Na Mwandishi Wetu, Tabora
MKUU
wa Mkoa wa Tabora Dk.Batilda Buriani ameipokea kwa mikono miwili
Taasisi ya Mama Ongea na Mwanao pamoja na Strong Women ambao wamefika
kwenye mkoa huo kwa ajili ya Kampeni ya Samia Nivishe Viatu 2022.
Lengo
kuu la Kampeni ya Samia Nivishe Viatu ni kwamba kila mtoto mwanafunzi
mwenye uhitaji anavaa kiatu cha Samia Suluhu na kampeni hiyo itafanyika
katika mikoa yote nchini kulingana na ratiba.
Akizungumza mbele
ya Mwenyekiti wa Taasisi ya Mama Ongea na Mwanao Steven Mengele maarufu
Steve Nyerere pamoja na wawakilishi wa Stong Women, Dk.Batilda amesema
kinachofanywa na taasisi hiyo kinadhihirisha sanaa ni kioo cha jamii.
“Ninyi
mmeangalia kupitia kazi mnazofanya za sanaa mkajua changamoto zilizoko
kwenye jamii na mkaguswa lakini mmeenda mbali zaidi kwa kuona jinsi gani
mtamshika mkono Mama Samia ili awafikie watanzania wenye matatizo.
“Na
mngeweza kupata viatu vya mtumba lakini mkasema mtanunua viatu vipya
ili mtoto wa kijijini kabisa ajue jinsi gani Mama Samia alivyokuwa na
mapenzi na Watanzania na mkasema basi mtapeleka viatu vipya.Niseme tu
kwa jinsi ambavyo mmefanya Mwenyezi Mungu akawazidishe riziki pale
mlipotoa , akawang’arishie nyota zenu katika kazi,”amesema Dk.Buriani.
Aidha
amesema kinachofanywa na taasisi ya Mama Ongea na Mwanao pamoja na
Strong Women ni funzo kubwa na wamefika Tabora kwenye mkoa wenye uhitaji
mkubwa.
“Tunavyokwenda huko vijijini tunaona changamoto kubwa na
tunasema tuone jinsi gani tutaweza kufanya mmoja mmoja lakini ninyi
mmekuja kikundi, mkiwa na maono makubwa ya kusambaza viatu hivi Tanzania
nzima, kwa hiyo mmeacha alama na tutatafuta wadau ili kuongeza nguvu
kwenye hili mnalolifanya.
“Niseme tu tumefurahi sana,
tumefarijika sana , tunashukuru na kwa hakika Mama Samia amewavisha
watoto wa Tabora kupitia ninyi wenzetu wa Mama Ongea na Mwanao kwa
kushirikiana na Strong Women na kweli mmeongea na wenetu hapa
Tabora,”amesisitiza Dk.Buriani.
Awali Mwenyekiti wa Taasisi ya
Mama Ongea na Mwanao Steve Nyerere alimueleza Dk.Buriani wamefika kwenye
mkoa huo na watakwenda vijijini kugawa viatu kwa wanafunzi wenye
uhitaji.
“Kwasababu hatutaki kukabidhi kiatu kwa Mwalimu Mkuu
kunakuwa na changamoto kidogo, hivyo sisi wenyewe ndio tunamvisha mtoto
kiatu na anaondoka nacho.Viatu vyenyewe ni hivi hapa mfano
wake(akaonesha) tukasema tuje tukuoneshe uvione ili tuendelee na kampeni
yetu kwenye mkoa wako,
Kwa hiyo Mimi na Wenzangu baada ya kupata
ridhaa yako Mkuu wa Mkoa tutaelekea katika Kata ya Ikongolo,Wilaya ya
Uyui katika shule ya Msingi Ikongolo kuwapelekea Wanafunzi wenye uhitaji
wa viatu vya Mama samia” alisema Steve.
Wanafunzi wa Shule ya Msingi Ikongolo Kata ya Ikongolo,Wilaya ya
Uyui wakifurahia viatu walivokabidhiwa na Taasisi ya Mama Ongea na Mwanao na Strong Women.
MKUU
wa Mkoa wa Tabora Dk.Batilda Buriani akizungumza wakati akiikaribisha
Taasisi ya Mama Ongea na Mwanao chini ya Mwenyekiti wake Steven Mengere
almaarufu Steve Nyerere wakiwa sambamba na Strong Women ambao walifika
kwenye mkoa huo kwa ajili ya Kampeni ya kutekeleza kampeni yao ya ‘Samia
Nivishe Viatu2022’.Pichani kulia ni Mwenyekiti wa taasisi ya Mama Ongea
na Mwanao Steven Mengere almaarufu Steve Nyerere
MKUU
wa Mkoa wa Tabora Dk.Batilda Buriani akiwa ameambatana na Mwenyekiti wa taasisi ya Mama Ongea na Mwanao Steven Mengere almaarufu Steve Nyerere mara baada ya kuwasili ofisi za Mkuu wa Mkoa mkoani Tabora kwa ajili ya kutekeleza kampeni yao ya ‘Samia Nivishe Viatu2022’.