Mkurugenzi wa shule ya mchepuo wa kiingireza ya Tumaini Senior iliyopo Monduli,Modest Bayo akizungumzia kuhusiana na programu hizo wanazotoa shuleni hapo kwa lengo ya kuwawezesha wanafunzi kujiajiri pindi wanapohitimu masomo yao.
Mwenyekiti wa chama cha walimu mkoa wa Arusha, Lotha Laizer akizungumza katika hafla hiyo ya wanafunzi wa shule ya Tumaini Senior kuonyesha bunifu zao wanazofanya shuleni hapo.
Wanafunzi wa shule ya sekondari ya mchepuo wa kiingireza ya Tumaini Senior iliyopo wilayani Monduli mkoani Arusha wakionyesha moja ya programu wanayofanya ya mafunzo kwa vitendo kuhusu maswala la DNA .
……………………………..
Julieth Laizer ,Arusha
Zaidi ya wanafunzi 200 wameweza kunufaika na programu ya elimu kwa vitendo (PBL) ambayo inawaandaa kuweza kujiajiri na kuondokana na changamoto za ajira pindi wanapohitimu kidato cha nne na cha sita.
Aidha programu hiyo ambayo inatolewa na shule ya mchepuo wa kiingireza ya sekondari Tumaini Senior iliyopo wilayani Monduli mkoani Arusha imeweza kuwanufaisha wanafunzi hao ambapo asilimia kubwa wameweza kuwa wabunifu kwa kutengeneza vitu mbalimbali kulingana na elimu waliyoipata.
Akizungumzia kuhusiana na programu hiyo katika hafla ya kuonyesha bunifu hizo ,Mkurugenzi wa shule hiyo, Modest Bayo amesema kuwa programu hiyo ilianzishwa shuleni hapo tangu mwaka 2016 ambapo programu hufanyika nje ya masomo ya darasani huku wanafunzi wakipata muda wa kujifunza kwa vitendo kulingana na uhitaji wao .
“Programu hiyo kwa njia ya vitendo imegawanyika katika ngazi mbalimbali ikiwemo utafiti kwa ajili ya malaria ,uandishi wa habari,na utafiti juu ya vinasaba (DNA) ambapo vyote hivyo tunafanya kwa vitendo huku kila mwanafunzi akionyesha jinsi alivyojifunza.”amesema.
Ameongeza kuwa, tangu kuanza kwa programu hiyo imeweza kuwajengea wanafunzi upeo mkubwa na uelewa katika uhalisia wa darasani ambapo kupitia programu hiyo imewasaidia wanafunzi wengi waliohitimu kuweza kujiajiri pindi wanapohitimu masomo yao huku nakusubiri kuendelea na masomo jambo ambalo linawafanya kuweza kuwa wabunifu na kuweza kuisaidia jamii inayowazunguka .
Naye Mwalimu mkuu wa shule hiyo,Sifael Martin amesema kuwa mbali na utafiti hizo pia wameweza kufanya utafiti katika maswala ya Google kwa kutumia kompyuta huku wakitengeneza Robot inaweza kuruka juu ikiendeshwa kwa njia ya programu ya drons.
Amesema kuwa, mbali na programu hiyo ya PDL wamekuwa wakitoa programu ya Stemm ambayo inamwezesha mwanafunzi kufundishwa maswala ya Kompyuta Science ambayo hujifunza lugha ya kompyuta katika kutengeneza programu ikiwemo website.
Kwa upande wake ,Mwenyekiti wa chama cha walimu mkoa wa Arusha, Lotha Laizer amesema kuwa, uwepo kwa programu hiyo mashuleni ni muhimu sana kwa wanafunzi kwani inawawezesha kuweza kujiajiri pindi wanapomaliza kwani anakuwa na ubunifu wake tayari ambao unamwezesha kujiajiri katika sekta mbalimbali.
Aidha ameomba serikali kuanzisha programu hiyo katika shule za serikali ili kuweza kuwaandaa wanafunzi kuweza kujiajiri na kuondokana na changamoto ya ajira ambayo imekuwa ni changamoto kubwa kwa wahitimu wengi na kuweza kujiajiri na kuwa wanasayansi wazuri wa kusaidia wengine.
Mmoja wa wanafunzi shuleni hapo,Given Malyango kidato cha nne anayefanya programu ya utafiti wa panya na vyura wanavyoweza kutumika kwa ajili ya kujifunzia kwa vitendo alisema kuwa, walianza kwa kufuga panya wawili ambao wanatumika kufanyia utafiti shuleni hapo ambapo wameweza kuwafuga wakazaliana na kuweza hukupatikana panya kumi na moja kwa sasa ambao wanatumika kwa ajili ya kufanyia utafiti shuleni hapo.