******************
Na Mwamvua Mwinyi
ALIYEWAHI kuwa Waziri wa Elimu nchini, Profesa Jumanne Maghembe ,amewaasa wanafunzi kujiwekea malengo tangu wakiwa shule kwani itakayowajenga kifikra kupambana kielimu kwa maisha yao baadae.
Maghembe aliyasema hayo Wilayani Mwanga Mkoani Kilimanjaro ,katika mahafali ya nane ya kidato cha nne Shule ya Sekondari ya Kiislamu ya Vuchama, ambapo wanafunzi 45 wanatarajia kuhitimu elimu ya Sekondari.
Alieleza, malengo ndio nguzo ya kuwajenga wanafunzi waweze kufanikiwa katika masomo yao kwani malengo Yao ndiyo maisha yao.
“Wengi wasiokuwa na malengo wanakuwa wanapoteza,katika kila mafanikio panahitaji malengo, bila lengo utawaacha wenzako wenye malengo wakiwa kwenye nafasi nzuri na baadae Kuwa na kazi na maisha mazuri huku wale wasio na malengo wakiishi wakitangatanga kutokana hawajui washike nini”
“Mtoto anahitaji elimu ili aweze kupambana na kushindana na wenzake sehemu nyingine, Msivunjike imani kuwa shule za Kiislamu hazifanyi vizuri badilisheni huo mtazamo ,na na wapongeza hapa mmeonyesha hamna ubaguzi mnawachukua watoto wote bila kubagua wote mnawaweka wanakuwa daraja moja,”alisema Maghembe.
Nae Meneja wa shule ya Sekondari Vuchama, Yasin Mfinanga alieleza shule imejipanga kufanya vizuri kwani wamewaandaa wanafunzi kwa ajili ya mitihani ya mwisho ya kidato cha nne ambayo watafanya hivi karibuni.
Mkuu wa Shule Jumanne Mkoga alisema , mwaka huu wanataka kufanya vizuri kwenye mtihani wa Taifa kwa kushika namba 10 bora kwani kuna baadhi masomo wamekuwa wa kwanza kimkoa.
Mkoga alisema ,masomo hayo ni jografia, kemia na baiolojia hivyo uhakika wa kushika nafasi hiyo na wamejipanga vizuri kwa kuwaandaa vizuri kitaaluma.
Akisoma risala ya wahitimu wa kidato cha nne Leila Msuya alisema kuwa shule yao imepata mafanikio ikiwa ni pamoja na kuongeza ufaulu ,kuboresha maktaba kununua vitabu na kuhifadhi mitihani ya miaka iliyopita ,kununua vifaa vya maabara ,mtaalamu na kuongeza jengo la kompyuta na kompyuta.