Mfugaji wa samaki na Mmliki wa Kampuni ya Sameki inayojihusisha na ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba Meck Sadick
Samaki aina ya sato wanaofugwa kwa njia ya vizimb
Vizimba vya kufugia samaki
…………………………………….
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Wafugaji wa samaki Mkoani Mwanza wameiomba Serikali kutenga maeneo kwaajili ya uzalishaji wa chakula cha samaki hatua itakayosaidia kupunguza gharama za kuagiza chakula hicho nje ya nchi.
Wakizungumza na Fullshangwe Blog baadhi ya wafugaji wa samaki kwa kutumia vizimba walisema hivi sasa wanalazimika kutumia Dola za Marekani 38,000 sawa na milioni 88.6 kuagiza kontena moja kutoka Dola 28,000 (sh 65.3 milioni) kabla vita ya Ukraine na Urusi haijaanza.
Meck Sadick ni miongoni mwa wafugaji wa samaki kwa njia ya vizimba Wilayani Sengerema, alisema endapo Serikali italeta wawekezaji kwenye eneo la chakula cha samaki itasaidia kufungua milango mingi kwa watu kuwekeza katika sekta hiyo hali itakayosaidia kupunguza uvuvi haramu.
Alisema ufugaji huo unatija ukilinganisha na ufugaji mwingine kutokana na mfugaji kuwa na uhakika wa kuvuna kile alichokipanda.
Sadick alisema ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba unalipa ambapo amewashauri watu wasiogope wala kukatishwa tamaa badala yake wajikite kwenye ufugaji huo ili waweze kujikwamua kiuchumi.
Alisema ufugaji huo ni bora na wa kisasa kutokana na eneo dogo kuzalisha samaki wengi huku suala la gharama za awali za mradi zikiwa hazikwepeki, ambapo ameeleza kuwa kizimba kimoja ni sh.milioni 20 zikihusisha vifaranga 10,000, gharama za ujenzi na vibali vyote.
MTAFITI
Kwa upande wake Mtafiti Mwandamizi kutoka Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) Mkoa wa Mwanza Hillary Mrosso, alisema ufugaji wa samaki ndio njia mbadala ya kuzalisha samaki ili kuziba pengo litokanalo na kupungua kwa samaki katika maji ya asili.
Alisema mseto wa ufugaji wa samaki na kilimo ni eneo lenye fursa ya kukuza uchumi wa bluu ambapo uzalishaji wa vyanzo mbadala vya protini ya kulishia samaki unahitaji kufanyiwa tafiti.
Alisema ubora wa mbegu na ongezeko la samaki vinatarajiwa kuongezaka kutokana na unafuu wa upatikanaji wa chakula na hivyo wafugaji kuwa na nafuu katika uendeshaji wa shughuli hizo na kupelekea ongezeko la uzalishaji wa samaki kupitia ufugaji utasaidia kuziba pengo la upungufu wa samaki wanaovuliwa katika maji ya asili.
HALI YA UWEKEZAJI
Akizungumzia hali ya uwekezaji katika sekta ya uvuvi Mkurugenzi wa Utafiti,Mipango na mifumo ya Taarifa kutoka katika kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Mafutah Bunini alisema wako kwenye mchakato wa kuvutia wawekezaji kuanzisha Viwanda vinavyozalisha chakula cha samaki wanaofugwa kwenye vizimba.
Alisema kwa sasa wanaendelea kutengeneza mazingira rafiki kwa wawekezaji ili kuwavutia kuwekeza nchini miundombinu itakayozalisha chakula cha samaki ili kuweza kuwapunguzia gharama wafugaji.
Aliongeza kuwa chakula cha uhakika kitakapokuwa kinapatikana nchini kitatasaidia kuongeza hamasa ya watu kufuga samaki hatua itakayosaidia kuongeza kipato kwa mtu mmoja mmoja na Taifa kwaujumla.
WASIMAMIZI WAKE
Serikali imejipanga kufanya Mpango wa matumizi bora ya ziwa Victoria ambao utaainisha maeneo ambayo yatatumika kufanya ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba ili kutoa nafasi kwa shughuli za uvuvi wa asili kuendelea bila kuwa na muingiliano.
Hayo yalibainishwa Septemba 27,2021 na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega alipotembelea eneo la Kampuni ya Kichina ya Tangreen iliyowekeza katika mradi wa ufugaji wa samaki kwa kutumia vizimba kandokando ya ziwa Victoria Jijini Mwanza.
Alisema ufugaji wa samaki ni wa muhimu na ndio utakaosaidia kukidhi mahitaji ya nchi ambayo ni tani kati ya 700,000 hadi 800,000 kwa mwaka ambapo kwa sasa zinapatikana tani 400,000 hadi 450,000 hivyo ufugaji ukifanyika kwa tija utasaidia kuchochea ongezeko la samaki nchini.
AFISA UVUVI
Afisa uvuvi Mkoa wa Mwanza Titus Kilo, alisema wafugaji wa samaki wamesaidia kutoa ajira kwa vijana sanjari nakuchangia pato la Taifa kwa kutoa ushuru pindi wanapokuwa wamevuna ambao unaelekezwa kwenye kusaidia kutekeleza shughuli mbalimbali za kimaendeleo katika Mkoa.
Alisema wafugaji wanatakiwa kutumia mbegu ambazo zimezalishwa kitaalumu ili waweze kupata uzalishaji mzuri utakaowasaidia kujikwamua kiuchumi.
MKUU WA MKOA
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mh. Adam Malima alisema Jiji hilo linazidi kukua kiuchumi kutokana na rasilimali zilizopo na kuwa kitovu cha biashara eneo la Nchi za Maziwa Makuu.
Alisema uchumi wa bluu unaotokana na ziwa Victoria umechangia kuinua kipato cha mtu mmoja mmoja,wafugaji wa samaki kwa njia ya vizimba,wavuvi na Viwanda kwa ujumla.
Malima alisema ili kuondokana na uvuvi wa kawaida unaotumia nguvu nyingi na kupata samaki wachache Mkoa umepiga hatua kwa kuwaelimisha Wananchi kutumia uvuvi wa kisasa na ufugaji samaki kwenye vizimba utakaoleta tija katika jamii.
“Ufugaji wa samaki kwa kutumia vizimba na mabwawa utatusaidia kupunguza purukushani kati ya Serikali na wavuvi haramu kutokana na samaki wengi kupatikana kupitia ufugaji hivyo watu hawataona haja ya kuhangaika na uvuvi usio na tija”, alisema Malima