Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Bw. Petro Lyatuu amewataka Wakuu wa Idara na Vitengo kusimamia vyema Sheria ya Manunuzi ya Umma wakati wa manunuzi alipokuwa akifunga Mafunzo ya Manunuzi na Ugavi yaliyokuwa yakiendeshwa na Wataalam kutoka Bodi ya Wataalam wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB) kwa Menejimenti ya Wizara hiyo yaliyofanyika kwa siku mbili Jijini Dodoma.Kutoka kulia ni Kaimu Mkurugenzi Idara ya Ununuzi na Ugavi, Bibi Cesilia Kasonga, katikati ni Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu, Bw. Orest Mushi.
Afisa Mwandamizi Masoko na Uhusiano, Shamim Mdee kutoka Bodi ya Wataalam wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB) akishukuru uongozi wa Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo kwa ushirikiano katika kufanikisha mafunzo yaliyokuwa yakiendeshwa na Wataalam wa Bodi hiyo kwa wakuu wa Idara na Vitengo yaliyofanyika Jijini Dodoma.Kulia kwake ni Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Michezo Bw. Yusuph Singo na kushoto ni Mkurugenzi Msaidizi Lugha, Bibi Leah Kihimbi.
Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Bw.Petro Lyatuu akimkabidhi Cheti Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Michezo Bw.Yusuph Singo mara baada ya kumaliza mafunzo ya Ununuzi na Ugavi yaliyokuwa yakitolewa na Wataalam kutoka Bodi ya Wataalam wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB) yaliyofanyika jijini Dodoma.
………………….
Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO
Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo imetakiwa kuendelea kuzingatia Sheria iliyoanzisha Bodi ya Wataalam wa Ununuzi na Ugavi namba 23 ya Mwaka 2017 ili kuweza kuandaa mikataba ambayo inazingatia maslahi ya Serikali.
Mkurugenzi wa Sera na Mipango Bw. Petro Lyatuu ameyasema hayo leo jijini Dodoma wakati alipomuwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara hiyo kufunga mafunzo ya siku mbili ya ununuzi na ugavi yaliyoandaliwa kwa ushirikiano wa wizara hiyo na Bodi ya Wataalam wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB).
Bw. Lyatuu amesema kuwa mafunzo hayo yataleta manufaa makubwa katika uandaaji wa mikataba pamoja na mchakato mzima wa manunuzi kwani mafunzo yamewakumbusha wahusika wa manunuzi majukumu yao, majukumu ya Bodi ya Zabuni pamoja na nguvu yake katika kuwashauri viongozi wao.
“Sote tunatambua kuwa takribani asilimia 90 ya fedha za Serikali zinaenda kwenye manunuzi hivyo natoa rai kwa wahusika kutumia sheria hii kama kitendea kazi kitakachowasaidia kuzingatia sharia na taratibu za ununuzi,” alisema Lyatuu.
Bw. Lyatuu ameongeza kuwa mafunzo hayo yamewasaidia kufahamu sheria na mlolongo mzima wa manunuzi ambao utaondoa changamoto katika ununuzi wa umma pamoja na kugundua baadhi ya mapungufu yaliyopo katika Sheria hiyo ikiwemo eneo linalohusu masuala ya adhabu na kutoa mapendekezo yao.
Aidha, ametoa rai kwa PSPTB kuandaa mafunzo kwa Wanasheria kwani ndio washauri Wakuu wa Viongozi wa Wizara pia ndio wanaohusika na kuangalia kama mikataba ya manunuzi imefata utaratibu.
Akimuwakilisha Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Ununuzi na Ugavi, Afisa Mwandamizi Masoko na Uhusiano kwa Umma, Shamim Mdee amefafanua kuwa PSPTB ndio taasisi inayohusika na utoaji wa mafunzo kwa watu wa ununuzi na ugavi pia ni moja ya taasisi ambayo inatakiwa kuishauri Serikali kama kuna mahali kuna ugumu kwenye sheria au mchakato mzima wa manunuzi ya umma.
Ameishukuru Wizara ya Habari kwa kushiriki kikamilifu katika semina hiyo na kutoa rai kwao kuendelea kuwa mabalozi wa taasisi hiyo kwa kuendelea kuyatumia vizuri mafunzo hayo katika mchakato mzima wa manunuzi ya umma.
Nae Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Sheria, Evod Kyando amesema kuwa mafunzo hayo yatawasaidia wanasheria kuweza kutoa maamuzi yatakayojikita katika taratibu za sheria ya manunuzi ambayo inazingatia thamani ya fedha na ubora wa huduma au bidhaa ambazo zinanunuliwa.