Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhe. Atupele Mwakibete, akihutubia washiriki wa
mkutano wa tatu wa mwaka wa Bodi ya Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi
(AQRB) (hawapo pichani), wakati alipofungua mkutano huo mkoani Dar es Salaam.
Msajili wa Bodi ya Wabuifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi (AQRB), Qs. Edwin
Nnunduma, akitoa taarifa ya Bodi katika mkutano wa tatu wa mwaka wa Wabunifu
Majengo na Wakadiriaji Majenzi uliofanyika mkoani Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhe. Atupele Mwakibete, akizungumza na Msajili
wa Bodi ya Wabuifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi (AQRB), Qs. Edwin Nnunduma
(kushoto), wakati alipokuwa akikagua mabanda katika mkutano wa tatu wa mwaka wa
watalam hao, mkoani Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhe. Atupele Mwakibete, akitizama moja ya kazi
wanazozifanya Wabuifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi wakati alipotembelea mabanda
yaliyopo katika mkutano wa tatu wa mwaka wa watalam hao, mkoani Dar es Salaam.
Mkutano huo umeandaliwa na Bodi ya Usajili wa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji
Majenzi (AQRB).
PICHA NA WUU
………………………….
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhe. Atupele Mwakibete, amezungumzia
umuhimu wa Bodi ya Usajili Wasanifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi (AQRB),
kuongeza idadi ya wataalam wa fani hiyo waliosajiliwa nchini.
Akifungua mkutano mkuu wa tatu wa AQRB jijini Dar es Salaam Mhe. Mwakibete
amesema Serikali itaendelea kutoa ufadhili wa mafunzo kwa vitendo kwa wahitimu wa
fani hiyo kila mwaka ili kuongeza idadi ya wataalamu hao wenye sifa nchini na hivyo
kuwawezesha kufanyakazi ndani na nje ya nchi.
”Serikali inatambua na kuthamini mchango wa Bodi ya Usajili wa Wabunifu Majengo na
Wakadiriaji Majenzi kwa uchumi na maendeleo ya nchi hivyo simamieni kikamilifu
sekta ya majenzi ili kuboresha miji na kuleta usalama wa majengo,”amesema Mwakibete
Mkutano huo unaoongozwa na mada kuu inayosema "uhifadhi wa majengo kwenye miji ya Afrika kwa sasa" unahudhuriwa na wataalamu mbalimbali katika sekta ya ujenzi kwa lengo la kubadilishana uzoefu na kupeana mbinu za kuhakikisha ubunifu majengo na ukadiriaji majenzi unakwenda sambamba na mabadiliko ya sayansi na teknolojia.
Mwakibete amewahakikishia wataalam hao kuwa Serikali itaendelea kutoa ufadhili huo
ili kuongeza idadi ya wataalamu wazawa na kuwa katika mwaka wa fedha 2022/23
Wizara imeidhinisha kiasi cha Shilingi milioni 550 kwa ajili ya Mpango wa Mafunzo ya
Wahitimu kwa Vitendo (EAPP).
Naibu Waziri Mwakibete ametoa wito kwa Bodi hiyo kuziangalia upya gharama za
usajili wa wanachama ili ziwe nafuu na hivyo kuwawezesha wataalam wenye sifa
kusajiliwa na kuwawazesha wananchi kutumia huduma za wataalam waliosajiliwa.
Mwakibete amesema kuanzia sasa wataalamu wote watahusishwa katika miradi ya ujenzi
na kwamba wizara yake imeunda timu maalumu kwa ajili ya kupitia miradi inayoendelea
na kutathmini mahitaji yanayotakiwa.
"Kuanzia sasa lazima wataalamu wote washirikishwe kwenye miradi, Serikali itatumia
wataalamu katika sekta zote ili kukidhi mahitaji ya makundi yote," amesema Mwakibete.
"Natoa rai kwa waendelezaji kuhakikisha wanatumia wataalamu katika miradi ya ‘force
account’. Serikali tunaamini kwamba force account inapunguza gharama kwa Serikali,
kwa hiyo hata nyinyi hamtakiwi kutupa tofauti kubwa," amesema Mwakibete.
Mwenyekiti wa Bodi ya AQRB, Dkt. Ludigija Bulamile, amesema kuna umuhimu wa
kushirikisha wataalamu wote katika utekelezaji wa miradi ili kuondoa changamoto
zinazojitokeza baada ya kukamilika kwa miradi husika.
Amesema miradi yote inatakiwa kuwa na wataalamu wote, wakiwamo wahandisi,
wakandarasi na wabunifu majengo na wakadiriaji majenzi ili kuzingatia mahitaji ya
makundi yote yatakayotumia miundombinu.
Dkt. Bulamile amesema mada zitakazowasilishwa kwenye mkutano huo zitajielekeza
kwenye umuhimu wa kuhifadhi majengo na kwamba majengo ya serikali yanatakiwa
kuishi kuanzia miaka 60 hadi 99.
Awali, akizungumza kwenye mkutano huo, Msajili wa Bodi ya AQRB, Qs. Edwin
Nnunduma, amesema Bodi hiyo imesajili wataalamu 1,329, kati yao, 1,295 ni wazawa na
34 ni wageni.
Amesema mwaka jana waliweka lengo la kusajili miradi 1,000 lakini waliweza kusajili
miradi 1,097 yenye thamani ya Sh4.5 trilioni.
Kuhusu wahitimu katika fani hiyo, Nnunduma amesema takribani wahitimu 250
wanahitimu masomo yao kila mwaka, lakini ni 150 pekee ndiyo wanajiunga na bodi hiyo
na kupata fursa ya kupata mafunzo kwa vitendo kwenye taasisi mbalimbali za umma na
binafsi.