**********************
MOROGORO
Kaimu Kamishna wa Uhifadhi TAWA, Mabula Misungwi Nyanda ameanza rasmi utekelezaji wa maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Mhe. Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa hivi Karibuni kuhusu kuwapandisha vyeo Maafisa na Askari waliodumu muda mrefu kazini bila kupanda cheo.
Kamishna Mabula amewatunuku na kuwapandisha vyeo jumla ya Maafisa 90 na Askari 146 wa TAWA idadi ambayo haijawahi kutokea tangu taasisi hiyo ianze kupandisha vyeo watumishi wake.
Akizungumza katika hafla hiyo iliyofanyika katika ofisi za Makao Makuu ya TAWA Mkoani Morogoro, Kamishna Mabula amewapongeza watumishi hao na kuwataka kufanya kazi Kwa bidii na kuwa mfano wa kuigwa Kwa wengine Ili kufikia malengo ya shirika.
Kamishna Mabula amesema Muundo mpya wa Utumishi wa shirika hilo, umetoa fursa Kwa Askari kupanda cheo Kwa kuzingatia vigezo mbalimbali kama vile, nidhamu, mwenendo mwema, utendaji uliotukuka, uzoefu kazini tofauti na Muundo wa zamani ambao ulizingatia kigezo Cha elimu pekee na hivyo kushusha morali ya watumishi walioshindwa kujiendeleza.
“Nimefarijika sana kuona miongoni wa Askari waliotunukiwa vyeo Leo hii, wapo Askari 126, ambao wamehudumu Kwa muda Mrefu bila kupanda cheo, ambao Leo wamepanda cheo kutoka Askari wa Uhifadhi daraja la tatu hadi Askari wa Uhifadhi daraja la kwanza” amesema
Aidha Kamishna Mabula ametoa rai Kwa watumishi Wote wa TAWA kufanya kazi Kwa bidii Kwa kuzingatia fursa za kimuundo na vigezo vilivyoanishwa kwenye Amri za Jumla za Jeshi la Uhifadhi vinavyoruhusu kupanda cheo.
Sambamba na hilo, Kamishna Mabula amesema sekta ya Uhifadhi wa Wanyamapori inakabiliwa na Changamoto mbalimbali ikiwemo ujangili, uvamizi wa maeneo ya hifadhi Kwa shughuli za kibinadamu na migogoro baina ya binadamu na Wanyamapori, hivyo ametoa maelekezo Kwa Maafisa na Askari wa TAWA kushirikiana na Wadau wa Uhifadhi Ili kuhakikisha Changamoto hizo zinaisha katika maeneo yaliyohifadhiwa.
Vilevile amewaagiza watumishi Wote wa TAWA kufanya kazi Kwa bidii Ili kuhakikisha matarajio ya Bodi ya Wakurugenzi ya TAWA iliyozinduliwa hivi Karibuni.