Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Mhe. Khamis Hamza Chillo akizungumza katika kikao na uongozi wa mkoa wa Simiyu kamati ya mawaziri 8 wa kisekta wanaoshughulikia migogoro ya Ardhi ya Vijiji 975.
Sehemu ya wananchi wa kata ya Ihusi –Bariadi mkoani Shinyanga wakiwa katika mkutano wa hadhara wakati kamati ya mawaziri 8 wa kisekta wanaoshughulikia migogoro ya Ardhi ya Vijiji 975 walipofika katika eneo hilo jana.
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Mhe. Khamis Hamza Chillo akiwasalimia wananchi wa kata ya Ihusi-Bariadi wakati kamati ya mawaziri 8 wa kisekta wanaoshughulikia migogoro ya Ardhi ya Vijiji 975 walipotembelea eneo hilo jana.
Waziri wa Ardhi Mhe. Dkt Angeline Mabula, Waziri wa Maliasilio na Utalii Pindi Chana (wa pili kulia) na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Mhe. Khamis Hamza Chillo (Kulia) wakicheza muziki na wananchi wa kata ya Ihusi-Bariadi wakati kamati ya mawaziri 8 wa kisekta wanaoshughulikia migogoro ya Ardhi ya Vijiji 975 walipotembelea eneo hilo jana. (PICHA NA WIZARA YA ARDHI)
………………………………………
Na Munir Shemweta, WANMM SIMIYU
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira Mhe.Khamis Hamza Chilo amewataka viongozi wa mikoa na wilaya nchini kwenda kuwafundisha wananchi namna bora ya kusimamia sheria na taratibu za utunzaji na uhifadhi wa vyanzo vya maji.
Pia ametaka viongozi hao kuelimisha namna ya kufuata na kutekeleza sheria zitakazolinda mazingira, ardhi na maliasili wakiwemo wanyama pori na mapori ya akiba.
Chillo alitoa kauli hiyo Oktoba 17, 2022 kwa nyakati tofauti wakati akizungumza na uongozi wa mkoa wa Simiyu pamoja na wananchi wa kata ya Ihusi-Bariadi,Mkoani Simiyu katika mkutano wa hadhara wakati kamati ya mawaziri 8 wa kisekta wanaoshughulikia migogoro ya Ardhi ya Vijiji 975.
Alisema, miongoni mwa vitu vikubwa ambavyo Kamati ya Mawaziri wa Wizara za Kisekta imebaini wakati wa ziara zake ni upungufu na uchache wa usimamizi wa seheria hasa zile sheria za mazingira.
Kwa mujibu wa Chillo moja ya njia sahihi ya kutatua migogoro ya matumizi ya ardhi bila kuleta taharuki kama ilivyoelekezwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ni kwenda kuwafundisha wananchi kipi kipo kwenye sheria .
‘’Twendeni kufundisha namna bora ya kusimamia sheria na taratibu za utunzaji na uhifadhi vyanzo vya maji, ni masafa gani wananchi wanatakiwa kufuga ama kujenga kutoka chanzo cha maji maana kinyume na hapo kila siku tutakuwa tunalia mazingira, maliasili, ardhi plus migogoro’’. Alisema Chillo
Naibu Waziri huyo Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulia Mazingira alibainisha kwa kusema kuwa, bila kutoa elimu ya namna ya kusimamia sheria na taratibu za utunzaji na uhifadhi mazingira serikali itaingia mzigo mkubwa wa kuzunguka, kusema na kueleza tu kwa sababu tu kuna mambo hayajasemwa mwanzo.
‘’Tukawaambie watu wetu watunze vyanzo vya maji kinyume na hapo hatutakuwa na maliasili, hatutakiwa na rasilimali kwa sababu vyanzo vya maji ni fahari yetu watanzania.
Kwa mujibu wa Naibu Waziri Chilo, mpaka mpaka kesho bado wapo watu wanalima kwenye vyanzo vya maji, lakini wapo pia wengine wanapelekea mifugo kwenye vyanzo hivyo huku wengine wakiendesha shughuli za uchimbaji madini ambapo matokeo yake ni kuharibu vyanzo vya maji.