Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, Kiria Laizer (kushoto) akimkabidhi shilingi 5,000 mwanafunzi wa stashahada ya utunzaji kumbukumbu ya nyaraka katika chuo cha utumishi wa umma Tanga, Maureen Laizer kwa ajili ya ada ya masomo yake.
*******************************
Na Mwandishi wetu, Mirerani
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, Kiria Laizer ameongoza harambee ndogo ya kumchangia mtoto yatima ambaye ni mwanafunzi wa chuo cha utumishi wa umma Tanga anayesomea diploma ya utunzaji kumbukumbu ya nyaraka.
Kiria, ameongoza shughuli ya kumchangia msichana huyo Maureen Laizer ambaye anaishi na mama yake kwenye kata ya Endiamtu na kufanikisha kupata shilingi 500,000.
Awali, harambee hiyo ngodo ilifanyika na kupatikana shilingi 200,000 ila Kiria akaongezea shilingi 300,000 na kupatikana shilingi 500,000 zitakazotumika kwenye masomo ya mwanafunzi huyo.
Kiria akizungumza kwenye shughuli hiyo ya harambee amesema kuchangia elimu ni jambo jema kwenye jamii kwani hivi sasa msingi mzuri wa watoto ni kupatiwa elimu.
“Mtoto huyu amejitahidi hadi kufikia hatua hii ya kuwa mwanafunzi wa chuo hivyo ni vyema akasaidiwa ili aweze kuhitimu masomo yake anayosomea mkoani Tanga,” amesema Kiria.
Mwenyekiti wa Mamlaka ya Mji mdogo wa Mirerani Adam Kobelo amewapongeza viongozi na wananchi waliochanga na pia Kiria kwa kufanikisha harambee hiyo ndogo kwa kutoa fedha zake binafsi shilingi 300,000.
Hata hivyo, Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro Dk Suleiman Serera amemtaka mwanafunzi huyo kuhakikisha anasoma kwa bidii ili aweze kutimiza ndoto zake na pia kutumikia Taifa hapo baadaye.
“Pia unapaswa kutambua kuwa hakuna haki isiyokuwa na wajibu, unachangiwa fedha za masomo lakini ofisa mtendaji wa kata atafuatilia huko chuoni kwenu ili kuangalia maendeleo yako,” amesema Dk Serera.
Kwa upande wake mwanafunzi huyo Maureen amemshukuru Mkuu huyo wa Wilaya, Mwenyekiti wa CCM na viongozi wote waliofanikisha yeye kuchangiwa na kupata fedha hizo za ada za masomo.
“Nawashukuru wote waliofanikisha mimi kupata msaada huu wa ada ya masomo na ninawaahidi kusoma kwa bidii kwenye masomo yangu huko chuoni Tanga,” amesema.