Majengo pacha ya mama na mtoto pamoja na upasuaji katika kituo cha afya Liganga Halmashauri ya wilaya Songea mkoani Ruvuma yakiwa yamekamilika kwa asilimia 100 kama yanavyoonekana.
Jengo la wagonjwa wa nje katika kituo cha Afya Liganga Halmashauri ya wilaya Songea likiwa tayari kwa matumizi baada ya Serikali kukamilisha ujenzi wa kituo hicho cha afya kwa gharama ya Sh.milioni 500.
Mganga Mkuu wa Halmashauri ya wilaya Songea Dkt Geofrey Kihaule wa tatu kushoto,mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha Selekano Magreth Haule wa tatu kulia na mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Sister Chrisma Ngonyani wa kwanza kulia na mchumi wa Halmashauri hiyo Christopher Ngwelalii wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya mafundi na viongozi wa kamati ya ujenzi wa kituo cha afya Liganga ambacho kimekamilika kwa asilimia 100.
…………………………….
Na Muhidin Amri,Songea
WANANCHI wa vijiji vitatu vya kata ya Liganga na vijiji vingine vinavyopakana na kata hiyo katika Halmashauri ya wilaya Songea,wanatarajiwa kuondokana na changamoto ya upatikanaji wa huduma ya afya waliyokuwa wanakabiliana nayo kwa muda mrefu, kufuatia ujenzi wa kituo cha afya kinachojengwa katika kata hiyo kukamilika kwa asilimia 98.
Mkuu wa idara ya afya,ustawi wa jamii na lishe wa Halmashauri hiyo Dkt Geofrey Kihaule alisema,kituo hicho kinajengwa katika kijiji cha Selekano ambapo kwa gharama ya Sh.milioni 500 ambazo zimetolewa na Serikali kwa awamu mbili.
Dkt Kihaule alisema,katika awamu ya kwanza serikali ilitoa kiasi cha Sh.milioni 250 ambazo zilitumika kujenga jengo la wagonjwa wa nje(OPD)maabara,na kichomoea taka ambapo majengo hayo yamekamilika kwa asilimia 100.
Alisema,majengo hayo yanatarajiwa kufunguliwa katika kipindi cha mwezi mmoja ujao na kuanza kutoa huduma kwa wagonjwa wa magonjwa ya nje wanaofika kwa ajili ya kupata huduma mbalimbali za matibabu.
Kwa mujibu wa Dkt Kihaule,watumishi watatu watakao fanya kazi katika kituo hicho wameshafika na kwa sasa wapo katika zahanati ndogo ya misheni ya Liganga wakisaidia kutoa huduma kwa wananchi huku wakisubiri kufunguliwa kwa kituo hicho.
Aidha alisema,katika awamu ya pili Halmashauri imepokea jumla ya Sh.milioni 250 kwa ajili ya kujenga majengo pacha ambayo ni ya huduma ya mama na mtoto,upasuaji pamoja na jengo la kufulia ambayo yote kwa sasa yamekamilika.
Dkt Kihaule,ameiomba serikali kuwasaidia kupata vifaa vikiwamo vya maabara mapema ili waweze kuanza kutoa huduma, kwani majengo yote yamekamilika na kinachosubiri ni kupata vifaa vya upasuaji,maabara na vitanda kwa ajili ya kulaza wagonjwa.
Alisema,kituo hicho kinatarajiwa kuwahudumia watu wengi zaidi kuliko kituo chochote cha afya katika Halmshauri ya wilaya Songea wakiwamo wafanyakazi zaidi ya elfu nne wa shamba la kahawa la kampuni ya Aviv Ltd ambao wengi wanaishi katika kijiji cha Liganga.
Dkt Kihaule alitaja wanufaika wengine ni wananchi wa kijiji cha Liganga,Seekano,wafungwa na askari wa gereza la Kitai,wafanyakazi wa migodi ya makaa ya mawe,wananchi wa kijiji cha Amanimakoro kilichopo wilaya jirani ya Mbinga, wananchi wa kijiji cha Mbinga Mhalule,Matomondo na Lipokela.
Alisema,kukamilika kwa kituo hicho ni ufumbuzi mkubwa sio kwa wananchi wa kata ya Liganga tu, bali hata kwa watu wengine wanaotumia barabara ya Songea-Mbinga ambao wakipata ajali na shida nyingine watakimbilia katika kituo hicho kwa ajili ya kupata msaada wa matibabu.
Mwenyekiti wa kijiji cha Selekano Magreth Haule,ameishukuru serikali kupitia Halmashauri hiyo kuwajengea kituo cha afya kwani awali walilazimika kutembea umbali mrefu na kutumia gharama kubwa Kwenda kupata matibabu maeneo ya mbali.
Amempongeza Mbunge wa JImbo la Peramiho na Waziri wa nchi ofisi ya Rais menejimenti ya utumishi wa umma na utawala bora Jenista Mhagama,kwa kazi nzuri anayofanya ya kuwahudumia wananchi wa jimbo hilo na kutafuta fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya Songea Neema Maghembe alisema,tayari wamepokea jumla ya watumishi 39 wa kada mbalimbali katika sekta ya afya ambao wamesharipoti na wanaendelea kufanya kazi ya kuwahudumia wananchi.
Maghembe alisema,katika kipindi cha mwaka mmoja wamepokea Sh.bilioni 1 zinazotokana na tozo kwa ajili ya kujenga vituo viwili vya afya katika kata ya Liganga na Mgazini.
Aidha alieleza kuwa, wamepokea fedha nyingine kiasi cha Sh.milioni 500 kwa ajili ya kujenga jengo la upasuaji na majengo mengine katika Hospitali ya Halmashauri iliyopo kijiji cha Mpitimbi ambayo imeshaanza kutoa huduma kwa wananchi wa Songea na wale wanaotoka nchi jirni ya Msumbiji.
Maghembe alisema, katika mkakati wa kusogeza huduma kwa wananchi wamefanikiwa kujenga zahanati katika kijiji cha Ndongosi kwa gharama ya Sh.milioni 50 na zahanati nyingine katika kijiji cha Makwaya kata ya Lilahi ambapo wananchi walilazimika Kwenda maeneo mengine kufuata matibabu.
Pia alisema, wamepokea kiasi Sh.milioni 104 ambazo zitatumika kuboresha mazingira ya kujifungulia kwa akina mama wajawazito katika zahanati mbalimbali ambapo kwa sasa wananchi wa maeneo hayo wanaendelea kufurahia huduma bora za afya.
Maghembe amewaasa wananchi kutumia zahanati,vituo vya afya na Hospitali zinazojengwa kwenda kupata huduma bora za afya kwani serikali inatumia fedha nyingi kwa ajili yao na kuachana na mira zilizopitwa na wakati zinazodai ukiwa mtu wa kwanza kupata huduma kwenye vituo na Hospitali zinazojengwa unaweza kupoteza maisha.