Kufuatia kutoridhishwa na thamani ya fedha iliyotumika katika kujenga miradi miwili ya Soko la Mazao lililopo Kata ya Makoka na Mnada wa Mifuko wa Kijiji cha Mbande wilayani Kongwa, Mkuu wa Wilaya hiyo Mhe, Deo Ndejembi ameiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU kufanya uchunguzi kwenye miradi hiyo.
DC Ndejembi ametoa agizo hilo wakati alipofanya ziara ya kukagua miradi hiyo inayojengwa kwa ushirikiano wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa pamoja na Ubalozi wa Denmark nchini.
” Hatujaridhishwa na money for value kwenye miradi hii, kiasi cha Shilingi Milioni 56 kilichotumika kwenye mradi wa Mnada na Milioni 200 zilizotumika mpaka sasa kwenye Soko la Mazao haziendani na hiki tulichokiona. Muonekano wa miradi hauakisi thamani ya fedha tunayoambiwa, hivyo naagiza TAKUKURU kufanya uchunguzi mara moja na kuniletea ripoti ili tujue ukweli na kama ni hatua tuchukue,” Amesema DC Ndejembi.
Katika ziara hiyo DC Ndejembi ameambatana na Wawakilishi wa Balozi wa Denmark ambapo aliwaomba pia kupitia Taasisi ya LIC kuweza kutoa sapoti yao kwenye ujenzi wa kiwanda cha maziwa ili kiweze kukamilika na kutoa ajira kwa kundi kubwa la vijana wa Kongwa pamoja na kuongeza mapato ndani ya Wilaya hiyo.
Nae Kiongozi wa Timu ya Maendeleo ya Biashara kutoka Ubalozi wa Denmark, Bi Jema Ngwale amemuahidi DC Ndejembi kuendelea kushirikiana nae katika kuwaletea maendeleo wananchi wa Kongwa.
” Suala la kiwanda hiki cha maziwa tumelichukua na naamini litakwisha, tunajua kikikamilika ni faida kwa Wananchi wa hapa kwenye ajira lakini pia itakuza uchumi wa Kongwa na hivyo kufanikisha azma ya Rais Magufuli katika kufikia uchumi wa kati kupitia viwanda, hivyo nakuahidi tumelichukua,” Amesema Bi Jema.