*********************
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), Mhandisi Victor H. Seff amemuondoa kwenye majukumu yake aliyekuwa Meneja wa TARURA Wilaya ya Kilombero kwa kushindwa kusimamia kikamilifu miradi ikiwemo ujenzi wa Boksi Kalavati katika Barabara ya Mawala-Mofu-Ikwambi Km 30 iliyopo Halmashauri ya Mlimba, Wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro.
Hayo yamejiri baada ya Kiongozi huyo kufanya ziara ya ukaguzi wa miradi wilayani Kilombero na kubaini mapungufu katika usimamizi wa miradi ikiwemo ujenzi wa boksi kalavati katika barabara ya Mawala-Mofu-Ikwambi ambalo limejengwa chini ya viwango vya mkataba hali iliyompelekea kumuondoa mara moja Meneja wa TARURA wa Wilaya hiyo.
“Nimekagua na kujiridhisha kwamba mradi huu umejengwa chini ya kiwango, kwakweli sijaridhishwa kabisa na usimamizi wa hapa, hivyo nimemuondoa kwenye nafasi yake kuanzia leo aliyekuwa Meneja wa TARURA Wilaya ya Kilombero na atapangiwa majukumu mengine”, alisema Mhandisi Seff.
Aidha, Mtendaji Mkuu amemtaka Mkandarasi aliyejenga mradi huo chini ya viwango vya mkataba kubomoa kwa gharama zake na kukamilisha ujenzi wa Boksi Kalavati jipya ndani ya kipindi cha mwezi mmoja.
Pia, Mhandisi Seff amewataka Mameneja wa TARURA nchi nzima kusimamia kikamilifu miradi kwenye maeneno yao na kwamba hatua kali zitachukuliwa kwa yeyote atayeshindwa kutimiza majukumu yake ili kuhakikisha fedha inayotolewa na Serikali inaendana na ubora wa miradi inayotekelezwa.
Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) unaendelea na kazi ya kusimamia ujenzi, ukarabati na matengenezo ya mtandao wa barabara za Wilaya wenye jumla ya KM 144,429.77 nchi nzima ili kuhakikisha wananchi wanazifikia huduma za kijamii na kuendeleza shughuli zao za kiuchumi.