Na Mwamvua Mwinyi, Chalinze
MBUNGE jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete, ameuelekeza Uongozi wa Halmashauri ya Chalinze na Shule ya msingi Chalinze Modern Islamic kutafuta jawabu ya changamoto ya mwanafunzi Iptisam Slim kuhusu kulalamika kubadilishiwa namba ya mtihani wake.
Sakata hilo lililoibuka asubuhi octoba 14 mwaka huu , Ridhiwani amewataka kuhakikisha jamii inapatiwa taarifa za ukweli kuhusu tukio zima na kama itakuwa kuna yeyote aliyehusika kuweka mazingira hayo ikiwa ni dhuruma kwa mwanafunzi ama kuchafua sura ya Shule basi hatua za msingi kupata haki zifuate.
“Nimepokea taarifa zinazomhusu Bint yetu , kuhusu shida iliyotokea kwenye Mitihani yake ya Darasa la Saba katika shule ya Msingi ya Chalinze Modern,Binafsi nieleze kwanza masikitiko kwa tukio zima maana linatupa nafasi ya kuhoji juu ya ukweli wa habari nzima, Si jema kwa Mwanafunzi, Shule wala Halmashauri yetu ya Chalinze. “
Ridhiwani alisema ,elimu ni kipaumbele cha Jimbo ,kusomesha watoto wa kike ndiyo njia ya ukombozi hivyo anaamini Halmashauri ambayo ndio yenye wajibu wa kusimamia Elimu watatoa taarifa punde kama alivyoelekeza.
“Tunaomba Utulivu wakati jambo hili linafanyiwa kazi hili tupate muafaka wake. Ninaamini Haki itatendeka kwa pande zote zinazohusika”