*******************
Na Mwamvua Mwinyi, Pwani
Oct 14
OFISA wa elimu Mkoani Pwani,Sara Mlaki na idara ya elimu msingi Chalinze wamekiri kupokea malalamiko kutoka kwa mtahiniwa katika shule ya msingi Chalinze Modern Islamic Iptisam Suleiman Slim akilalamika kuchakachuliwa namba yake ya mtihani hivyo kuhofia matokeo ya mtihani kuwa mabaya.
Wakizungumzia juu ya taarifa za mtahiniwa huyo , walieleza taarifa wamepokea tangu octoba 13 na hatua za uchunguzi zinafanyika ili sheria iweze kuchukua mkondo wake.
Sara alieleza, wanafuatilia na taarifa za kiuchunguzi zikikamilika, msemaji atatolea ufafanuzi wa kina.
“Tumepokea malalamiko hayo ,Ni kweli kinachosambazwa Ila tunafuatilia ,tunafuatilia ,Kama Kuna lolote litatolewa ufafanuzi”alisisitiza.
Nae ofisa elimu msingi Chalinze,Miriam Kihio alieleza ,wamefikishiwa taarifa hizo Ila ikifikia hatua ya mtihani changamoto yoyote idara inakuwa sio msemaji.
“Idara sio wasemaji ,nimepokea malalamiko Lakini siwezi kumzungumzia lolote,msemaji ni Mwenyekiti wa kamati ya mtihani wa wilaya ambae ni Mkurugenzi wa Halmashauri Chalinze, pamoja na mkoa “alisema Kihio.
IPTISAM
Awali Iptisam alitoa kilio chake akidai octoba 5-6 mwaka huu walifanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi ambapo ,alipoingia darasani alipangiwa namba 40 wakati karatasi ya kusaini inapita chakushangaza akakuta jina lake lipo namba 39.
“Nikamuuliza msimamizi wa mtihani mbona namba ni 40 na karatasi ya kusaini nipo namba 39 , msimamizi akasema hili suala tutalishughulikia NECTA watarekebisha “
“Nilifanya mitihani mitano kwa namba 40 mtihani wa English,math, kiswahili,civics na science” mtihani wa mwisho social studies nikaambiwa nibadilishane ,nikafanya mtihani kwa namba halisi ya 39 “
“Baada ya mtihani baadhi ya wanafunzi tuliitwa na teacher Kijangwa ,tukaambiwa tusiseme yaliyotokea kokote hata kwa wazazi wasijue”
Iptisam aliiomba Wizara ya elimu , Waziri wa elimu ,maafisa elimu wilaya na mkoa kumsaidia kupata haki yake kwani alikuwa akifanya vizuri darasani na alikuwa akifaulu kumi bora na mtihani wa moko wilaya alishika namba moja.
Wasiwasi wake aliyebadilishiwa namba alikuwa hayupo vizuri kwenye taaluma darasani anaogopa asibadilishiwe matokeo yakawa amefeli.
CCM WILAYA
Kwa upande wa Chama Cha Mapinduzi CCM Bagamoyo, Mwenyekiti wa CCM Alhaj Sharif Zahoro alisema wiki ya mtoto kike Duniani kila kona ilipaza sauti ikizungumzia haki ya mtoto wa kike kupata elimu,Jambo ambalo jamii,walimu, wanatakiwa kumshika mkono mtoto wa kike afikie ndoto zake pasipo kumkwamisha.
Alieleza, mtoto wa kike asikatishwe tamaa ,asiwe sehemu ya kuonekana hafai kusoma au kufaulu kwani nao wana haki ya kupata elimu na kufaulu mitihani yao.
“Kam Kuna ukweli wa Jambo hili,na shule au walimu wamefanya mchezo huo kiukweli nimesikitika sana, Lazima uchunguzi ufanyike na ikibainika Kuwa wamehusika kuchakachua mtihani wa mtahiniwa huyo ,basi hatua zichukuliwe dhidi Yao”alieleza Sharif.
BARAZA LA MTIHANI(NECTA)
Baraza la mtihani Tanzania NECTA , limeeleza limeona taarifa inayosambaa mitandao ya kijamii,ikionyesha mtahiniwa Iptisam Slim akisema kwamba abadilishiwa namba yake ya mtihani wakati anafanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi.
Ofisa habari na uhusiano John Nchimbi alifafanua , Baraza la mtihani linafanyia kazi taarifa hii ili kuhakikisha mtahiniwa anapata haki yake.
Hata hivyo Mkurugenzi wa Chalinze Modern Islamic Omary Ismail, alipopigiwa simu kumzungumzia ukweli wowote kuhusu malalamiko hayo yanayohusisha shule hiyo ambayo inarekodi ya kufanya vizuri wilaya na mkoa,hakupokea simu yake japo ilikuwa hewani.