Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (katikati) akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Nakalonji wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge (MKURABITA) katika Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea.
Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea, Mhe. Hashim Komba akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi kuzungumza na wananchi wa Kijiji cha Nakalonji wakati ziara ya kikazi ya Naibu Waziri huo iliyokuwa na lengo la kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge (MKURABITA) katika Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea.
Mwakilishi wa Mratibu wa MKURABITA, Bw. Mujungu Mwasyenene akitoa taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya MKURABITA kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais – UTUMISHI na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri huyo yenye lengo la kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge (MKURABITA) Wilayani Nachingwea.
Baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Mbondo wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (hayupo pichani), wakati wa ziara yake ya kikazi ya Naibu Waziri huyo yenye lengo la kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge (MKURABITA) katika Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea.
Mmoja wa wananchi wa Kijiji cha Mbondo, Bw. Waziri Ally Pelenje akieleza namna alivyonufaika na MKURABITA, mara baada ya Naibu Waziri Ndejembi kuhitimisha ziara yake ya kikazi iliyolenga kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge (MKURABITA) katika Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea.
Mwananchi wa Kijiji cha Mbondo, Bw. Koini Mwanjisi akieleza namna alivyonufaika na MKURABITA, mara baada ya Naibu Waziri Ndejembi kuhitimisha ziara yake ya kikazi iliyolenga kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge (MKURABITA) katika Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akikata utepe kuzindua masijala ya ardhi katika Kijiji cha Mbondo, wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge (MKURABITA) katika Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea.
****************************
Na. James K. Mwanamyoto-Nachingwea
Tarehe 13 Oktoba, 2022
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi ameilekeza MKURABITA kutoa elimu ya namna bora wananchi wa Vijiji vya Mbondo na Nakalonji wilayani Nachingwea wataweza kutumia hati miliki za ardhi za kimila kuomba mikopo katika taasisi za kifedha itakayowawezesha kufanya shughuli mbalimbali za kiuchumi zitakazoboresha maisha ya wananchi wa vijiji hivyo.
Mhe. Ndejembi ametoa maelekezo hayo kwa MKURABITA mara baada ya kuzindua masijala za ardhi zilizojengwa na MKURABITA katika Vijiji vya Mbondo na Nakalonji wilayani Nachingwea, akiwa kwenye ziara yake ya kikazi iliyolenga kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge (MKURABITA) katika Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea.
Mhe. Ndejembi amesema, taasisi za kifedha kama benki ya NMB na CRDB wanazitambua hati miliki za kimila hivyo ni wajibu wa MKURABITA kuhakikisha wananchi wa Vijiji vya Mbondo na Nakalonji waliorasimishiwa ardhi na kupatiwa hati miliki, wanapatiwa elimu ya namna gani watazitumia hati hizo kupata mikopo itakayowawezesha kujishughulisha na kilimo na ujasiriamali ili wapate maendeleo.
“Wananchi wa Vijiji vya Mbondo na Nakalonji wana ardhi inayowawezesha kulima korosho ya kutosha, hivyo wakipata fedha za mikopo kutoka katika taasisi za kifedha wataweza kujishughulisha na kilimo cha korosho chenye tija katika kuwaongezea kipato,” Mhe. Ndejembi amesisitiza.
Aidha, Mhe. Ndejembi amewaasa wananchi wa Vijiji vya Mbondo na Nakalonji kutotumia hati walizopatiwa na MKURABITA kukopa fedha na kuzitumia kwa anasa kwani pindi watakaposhindwa kurejesha mikopo hiyo ardhi zao zitataifishwa na taasisi za kifedha.
Mmoja wa wananchi wa Kijiji cha Mbondo, Bw. Waziri Ally Pelenje amemshukuru Mhe. Ndejembi kwa kuielekeza MKURABITA kuwapatia elimu ya namna bora watakavyonufaika na hati miliki za kimila walizopatiwa na Serikali kupitia MKURABITA na kuahidi kuitumia vema elimu atakayoipata kujipatia maendeleo.
Naye, Mwananchi mwingine wa Kijiji cha Mbondo, Bw. Koini Mwanjisi ameishukuru Serikali kwa kumuwezesha kupata hati miliki kwani imemsaidia kumuondolea migogoro ya mipaka ya ardhi aliyokuwa akikabiliana nayo, na kuongeza kuwa anamshukuru pia Mhe. Ndejembi kwa kuelekeza wapatiwe elimu ya kuzitumia vizuri hati hizo ili wapate mikopo itakayowawezesha kuendesha shughuli mbalimbali za kiuchumi.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa shughuli za MKURABITA, Mwakilishi wa Mratibu wa MKURABITA, Bw. Mujungu Mwasyenene amesema masijala za ardhi zilizojengwa na MKURABITA zimelenga kutunza hati ambazo wananchi walirasimishiwa mashamba yao, na kuongeza kuwa majengo hayo yatatoa huduma mbalimbali kwa wananchi wa Vijiji vya Mbondo na Nakalonji kwani yamejumuisha ofisi za Watendaji wa Vijiji, ofisi ya Watendaji Kata, ofisi za Maafisa Ugani na kumbi kwa ajili ya kuendeshea mikutano.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea, Mhe. Hashim Komba amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuiwezesha MKURABITA kupima mashamba na kuwapatia hati miliki za kimila wananchi katika vijiji vya Mbondo, Nakalonji na Nahimba vilivyopo katika wilaya yake.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amehitimisha ziara yake ya kikazi ya siku tatu mkoani Lindi, iliyolenga kutatua changamoto za watumishi wa umma, kuhimiza uwajibikaji,ikiwa ni pamoja na kukagua utekelezaji wa shughuli za TASAF na MKURABITA.