Serikali inakamilisha ujenzi wa Chuo cha Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VET) cha Mkoa wa Simiyu ambacho kinajengwa kwa fedha za Mpango wva Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO 19.
Akizungumza alipotembelea Chuo hicho kukagua maendeleo ya Ujenzi, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesema ujenzi wa chuo hicho utagharimu zaidi ya shilingi bilioni tano na ujenzi unatarajiwa kukamilika ifikamo mwezi Novemba, mwaka huu.
Prof. Adolf Mkenda amesema katika awamu hii ya kwanza yanajengwa majengo 25 ambayo yanapaswa kukamilika kwa haraka ili yaanze kutumika kwani ujenzi huo mpaka sasa upo nje ya muda kutokana na changamoto mbalimbali zilizojitokeza wakati wa kuanza mradi.
“Mradi huu upo nyuma ya muda kutokana na changamoto ambazo hazikuweza kuzuilika, lakini kwa sasa tunapaswa kufanya kazi usiku na mchana ili ukamilike mapema na kuwezesha vijana wa Simiyu kuja hapa kupata ujuzi” amesema Prof Mkenda.
Aidha, Kiongozi huyo ameutaka uongozi wa Chuo cha Ufundi Arusha ambao ndio wasimamizi wa mradi huo kufika katika eneo hilo kuangalia changamoto zilizojitokeza katika ujenzi huo na kuzitafutia ufumbuzi na zile ambazo haziwezi kutatuliwa zitolewe taarifa ili kuboresha mapungufu hayo katika miradi mingine kama hiyo.
Pia, Waziri Mkenda ameielekeza Mamlaka ya Elimu ya Ufundi na Mafunzo Stadi (VETA) kujipanga namna bora ya kuhakikisha ujenzi wa Vyuo 64 vipya vya Wilaya unatekelezwa kwa viwango na kwa wakati, ikiwemo kutumia wakandarasi kwa kutangaza zabuni za ujenzi kwa wakandarasi wa Sekta binafsi kwa baadhi ya vyuo na vingine kutumia ” force account” ili kufikia lengo la kukamilisha ndani ya Mwaka huu wa Fedha.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Bariadi Jina Lupakisyo Kapange amemshukuru Rais Samia na Wizara ya Elimu kwa kupeleka mradi wa ujenzi wa Chuo hicho katika mkoa huo ambacho kitasaidia kuwapatia ujuzi vijana.
Mshauri elekezi kutoka Chuo cha ufundi Arusha Mhandisi Jalalya Mabojano amemweleza Waziri kuwa mradi huo wa awamu ya kwanza unajenga miundombunu ya Jengo la Utawala, Maktaba, Jengo madarasa, mabweni manne, nyumba tano za watumish, Karakana sita na miundombinu ya vyoo.
Chuo cha VETA mkoa wa Simiyu ni kati ya Vyuo vinne vya Mikoa ambavyo vipo katika hatua za kukamilika ili vianze kudahili wanafunzi. Vyuo vingine vya Mikoa vinavyojengwa ni Njombe, Geita na Rukwa na vitakapokamilika itawezesha mikoa 25 kuwa na vyuo hivyo isipokuwa Mkoa mmoja wa Songwe.