Na Mwamvua Mwinyi, Pwani
WAZIRI wa Nchi ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira alhaj,Dkt.Selemani Jafo amekemea watendaji wa Serikali wanaofanya urasimu katika kuchelewesha nyaraka za wawekezaji ili kuwekeza nchini.
Aidha ameeleza Tanzania ni nchi ya mfano yenye amani na ni salama kwa Uwekezaji ambapo pia imejipanga kimkakati kwa ajili ya kuvutia wawekezaji hususan wa nje ya nchi.
Pamoja na hayo, ametoa rai kwa wawekezaji Mkoani Pwani kuacha tabia ya kufungua ofisi na kulipa ushuru wa huduma (Service levy)nje ya mkoa hali inayochangia kushusha mapato ya halmashauri za mkoa huo.
Ameyasema hayo wakati akifungua Kongamano la Biashara na uwekezaji Mkoani Pwani lililofanyika Ukumbi chuo Cha Mwalimu Nyerere kilichopo Kwamfipa Kibaha Mjini,lililohudhuriwa na washiriki wawekezaji 220 kati ya 250 waliotarajiwa.
Alieleza ,vikwazo vinavyofanywa na baadhi ya watendaji hao zinakwamisha juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan ambae kishatumia nguvu kubwa kuitangaza nchi.
Jafo alieleza Serikali imejidhatiti katika kuinua sekta ya uwekezaji na ujenzi wa viwanda ni salama hivyo wawekezaji wasiwe na hofu katika kuendeleza shughuli zao.
Alisema Kuwa ,Rais Samia Suluhu Hassan amejipambanua kuitangaza nchi katika masuala mbalimbali ya uwekezaji na kuleta matokeo chanya.
“Nchi imeweka Mazingira Bora ya uwekezaji katika sekta ya miundombinu ya barabara ,kwa kufungua na kuunganisha barabara za mikoa ,wilaya ili kuwarahisishia wawekezaji kusafirisha bidhaa na malighafi zao kirahisi bila kero ,imeunganisha usafiri wa reli kwa kujenga reli ya kisasa (Standard gauge)mradi ambao Rais Samia anauendeleza kuhakikisha unamalizika na kuleta tija”alifafanua Jafo.
Jafo alieleza pia wanaotembelea nchini wamethibitisha kuimarika kwa usambazaji wa maji kupitia Mamlaka ya maji safi na usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) na RUWASA ,na usambazaji wa Nishati ya umeme.
Alieleza,hadi kukamilika kwa mradi mkubwa wa umeme Stigo huko Rufiji mradi ambao ukikamilika utazalisha megawatts 2,115 na ukikamilika utagharimu kiasi cha sh.trilion 6.5.
Vilevile upo Mradi mkubwa wa Bandari kavu Kwala , maeneo ya uwekezaji Kazimzumbwi-Kisarawe , Bagamoyo , Mkuranga,Mafia kisiwa cha utalii kwa uwekezaji wa uchumi wa bluu.
Vilevile aliielekeza Wizara ya Viwanda na Biashara kushirikiana na Serikali Mkoani Pwani kuandaa kongamano la Uwekezaji na Biashara la Kitaifa litakalokuwa endelevu ili mikoa mingine ipate fursa ya kujifunza pamoja na kupanua wigo wa masuala ya uwekezaji kwa sauti moja.
Alishauri maonyesho yaendelee na yawe ya kudumu kwa ajili ya masuala ya uwekezaji.
Alimpongeza mkuu wa mkoa wa Pwani alhaj Abubakari Kunenge, kuyaendeleza yaliyoanzishwa na wakuu wa mikoa waliopita na yeye kuboresha maonyesho ya tatu ya wiki ya biashara na uwekezaji na kuweka nakshi zaidi kuongeza Kongamano la biashara na uwekezaji.
Nae Mkuu wa mkoa wa Pwani alhaj Abubakari Kunenge, alisema kuwa hadi sasa mkoa una kongani za viwanda 23 ambazo zimetengwa kwa ajili ya kujenga viwanda.
Alieleza ,kongani hizo ni pamoja na SINOTAN ambayo itajengwa viwanda 350 katika eneo lenye hekari 2,500.
Kunenge alifafanua kwamba ,upande wa viwanda vipo 1,460 kati ya hivyo 90 ni vikubwa.
Kwa upande wa Mwekezaji mkubwa Kwala Kibaha Vijijini,kutoka Kongani ya SINOTAN Jensen Huang alieleza ,mradi huo ni mkubwa Afrika ,unatarajia kuwa na ajira zaidi ya 100,000 na kujenga viwanda 350.
Alisema ni mradi utakaochukua miaka mitano ambapo awamu ya kwanza utachukua miaka miwili na awamu ya pili miaka mitatu.