Adeladius Makwega-MAKOLE
Siku moja nilikuwa nasafiri kutokea Dodoma kuelekea Tanga, kwa kuwa siku hiyo usafiri ulikuwa unasumbua sana iliniladhimu kuunganisha magari tangu Dodoma hadi Chalinze kwanza, niliposhuka Chalinze jua lilikuwa limezama huku mji huu ukiwa umechangamka mno.
Hata nilipofika hapa usafiri pia ulikuwa mgumu mno, nilisubiri kwa saa kadhaa na baadaye ilikuja gari moja ndogo ya ndugu mmoja ambaye alitufanyia hisani kutuchukua abiria kadhaa lakini hisani yake hiyo haikuweza kupunguza abiria waliopo stendi.
Gari nililopanda nilibaini lilikuwa la kiafisaliafisali, ndani yake walikuwapo watu wengine wawili, dereva akawa watatu mie na mwezangu tukawa jumla watu watano. Wakati tunajipanga namna ya kukaa vizuri, kwanza tuliiweka mizigo yetu ya mikononi yakiwa mabegi kadhaa na mie mwanakwetu nilikuwa boksi moja dogo.
Ndugu mmoja niliyemkuta ndani ya gari akaniuliza hilo boksi lako umebeba nini? Nilijibu, Nimebeba zabibu, akaniambia weka hapo katikati ya kiti cha dereva, kweli nikafanya hivyo. Akaniuliza umetoka nazo Dodoma? Nilimjibu naam, nawapelekea wanangu huko Tanga, kwa maana Tanga tajiri wa matunda lakini fukara wa zabibu.
Ndugu huyu akasema yeye ni mfanyabiashara wa zabibu na kwa mwaka 2022 zabibu zimezaa sana kwa kuwa ni mwaka wa mvua chache. “Hivi tunavyoongea nimetoka kuupokea mzigo wangu wa zabibu kutoka Dodoma ulipelekwa Dar es Salaam. Hapa nakwenda Arusha kuupokea mzigo wangu mwingine umepakiwa Dodoma na umeanza safari kwetu Arusha zabibu zina pesa sana.”
Nikampongezi ndugu yetu huyu kwa kufanya biashara hii akisema kuwa mwaka huu watapata pesa nyingi, nilimpa heko kwa kuchagua biashara hii ya msimu akisema msimu ukiiisha huwa anafanya biashara zingine.
Ndugu huyu akasema kuwa hata kama unawapelekea wanao jitahidi sana kuwapa zabibu kiasi kidogo usiwape nyingi kwa wakati mmoja, zinalewesha sana hizi. Nikauliza kweli? Ndugu huyu akasema ni kweli kabisa hakuna utani katika hili.
“Wakati ninaanza biashara hii nilijifunza jambo moja kubwa sana, wakati wa mavuno ukifika nilikuwa nasimamia kuvuna, kwa kuwa nilikuwa mgeni nilikuwa navuna huku nakula zabibi kidogo kidogo, baada ya muda kidogo naenda kulala nikiwaacha vijana wa kuvuna wakiendelea. Nikija kuzinduka nilibaini kuwa mzigo wangu ulikuwa pungufu mno.”
Nilijiuliza maswali shida nini hata gari likija kupakia lilikuwa nusu ya mzigo haupo nikawa napata hasara mno. Jambo hilo lilimsumbua hadi alipokuja kuambiwa kuwa wakati wa kuvuna zabibu mwiko mkubwa hautakiwi kula na kama unahitaji kula zabibu ziliwe wakati zoezi la kuvuna limekamilika.
Nikamuuliza ni zabibu zote sharti ni hilo hilo? Ndugu huyu akasema ndiyo tena zile zabibu nyeupe zenyewe ni kali zaidi, kubwa ni kutokuzila kabisa wakati wa kuvuna maana ukifanya hivyo mwanakwertu utakula wa chuya.
Vijana wa kigogo ni wajanja sana watakwambia mzee chukua zabibu hii ni tamu zaidi ya ile utapewa kitita cha kwanza utakila utakimaliza utapewa cha pili utakimaliza ukipewa cha tatu mwanakwetu ukikimaliza hali itabadilika.
“Sasa hivi nimewambia wadogo zangu ambao wananisimamia kuvuna, kula kula zaibibu wakati wa kuvuna huo ndiyo mwiko wake, kula baada ya kumaliza zoezi.” Alisema ndugu huyu.
Dereva wa gari hili akasema siyo katika kuvuna zabibu tu hata hata katika mambo ya uongozi jamii, taasaisi , shirika hata serikalini walio chini wanakutazama mkubwa wewe ukoje kama unapenda kuonja onja iwe pesa au tamaa yoyote. Wakitambua kuwa wewe ni mwanachama wa tamaa watakuwa wanakuletea letea kidogo kidogo, tambua kuwa na wao wanaiba ukishazoea utalewa na mwisho wa siku hamuwezi kuvuna chochote.
“Hamuwezi kufikia malengo yenu, mtakwama tu maana mtakuwa ni nyumba ya hasara kila uchao.”
Mwanakwetu nilifika Tanga salama salimini na mzigo wangu wa zabibu mkononi na kuwapa wanangu kidogo kiogo kuogopa ule ulevi wa zabibu kama walivyoniambia ndugu zangu hawa na simulizi ya uwoga wa kuvuna hasara na Tanga tajiri matunda.