Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) imeteuliwa kwa kipindi cha pili kuwa Mjumbe wa Bodi ya Wakaguzi wa Nje (BoEA) wa Umoja wa Afrika (AU) ikiwa ni miongoni mwa nchi kumi na moja (11) za Afrika zitakazofanya kazi ya kukagua Hesabu za Umoja wa Afrika.
Akizungumzia uteuzi huo, Katibu Mtendaji wa Bodi ya Wakaguzi wa Nje wa AU (BoEA), Bw. Dinberu Mulugeta Abebe amenukuliwa akisema, “Ninayo heshima kuwasilisha uamuzi wa Baraza la Utendaji kuhusu uteuzi wa Bodi ya Wakaguzi wa Nje wa AU, kwa miaka miwili ya fedha 2022 na 2023, kwa ajili ya Ukaguzi wa Hesabu za Fedha za Umoja wa Afrika.”
Kwa uteuzi huo kwenye Bodi ya BoEA, Wakaguzi kutoka Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi Tanzania (NAOT) chini ya usimamizi wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Bw. Charles E. Kichere, watashiriki katika kazi ya kukagua hesabu za Umoja wa Afrika kwa kipindi cha miaka miwili ya fedha 2022 na 2023.
Wakuu wa Taasisi za Juu za Ukaguzi walioteuliwa kuingia kwenye Bodi ya Wakaguzi wa Nje wa AU (BoEA) kwa mujibu wa Kanuni ya 98 ya Kanuni za Fedha za AU wanatoka katika Mataifa ya Tanzania ikiwakilisha nchi za Afrika Mashariki, Equatorial Guinea-Afrika ya Kati, Eswatini-Kusini mwa Afrika na Jamhuri ya Côte d’Ivoire ambayo inawakilisha nchi za Afrika Magharibi. Wakuu hao wa Taasisi wataungana na Wakaguzi Wakuu sita (6) kutoka nchi wanachama wa kudumu (first tier countries) ambazo ni mataifa ya Afrika ya Kusini, Algeria, Libya, Misri, Morocco, na Nigeria katika kuunda Bodi hiyo ya Ukaguzi.
Uteuzi wa Tanzania kwa mara ya pili kwenye Bodi ya Wakaguzi wa Nje wa Umoja wa Afrika ni uthibitisho wa imani kubwa waliyonayo wadau wa ndani na nje ya nchi hususani katika Umoja wa Afrika kwenye kazi za Ukaguzi zinazofanywa kwa umahiri mkubwa na Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi kwa kuzingatia utaalamu, uadilifu, ubunifu na matokeo yenye kuleta mabadiliko katika malengo ya kazi za Ukaguzi.