Na Mwamvua Mwinyi, Pwani
Kiwanda cha Sukari Bagamoyo, Mkoani Pwani kimeanza uzalishaji wa sukari na kuingiza sokoni sukari yake kwa kuuza jumla jumla kwa tani 10,mifuko 200 na kilo 50 hadi 25.
Aidha kutokana na mwamko wa wateja kununua sukari hiyo , kiwanda kinalenga kuanza kuingiza mijini na mitaani sukari hiyo kwa kuiuza rejareja kuanzia kilo 20, kilo moja,nusu na robo kilo ifikapo mwezi ujao.
Akielezea juu ya uwekezaji huo, katika maonyesho ya tatu ya wiki ya biashara na uwekezaji Mkoani Pwani yanayofanyika Mailmoja, Kibaha Mjini , katika banda la (Bakhresa group), Bagamoyo Sugar ,Msaidizi wa maabara Bagamoyo Sugar Nasra Mobutu alieleza , uzalishaji na kuingiza bidhaa sokoni wameanza rasmi Juni mwaka huu.
“Uzalishaji wa sukari hii unatokana na kulima miwa kwenye shamba letu la BAKHRESA tulilopatiwa na Serikali kwa ajili ya kilimo Cha miwa na uzalishaji sukari lenye hekari 10,000 wilayani Bagamoyo”
” Uvunaji na uzalishaji ni wa aina mbili kwa kutumia mashine tunapata tani 800 na kupitia watu tunapata tani 1,200 kwa siku “.
Nasra alibainisha, kwa siku wanazalisha tani 2,000 ya sukari ,kwa mwaka tani zaidi ya 17,000 huku kiwango cha miwa kwa mwaka wanavuna tani 175,000.
Mfanyabiashara mkubwa nchini Bakhresa alipatiwa shamba la hekari 10,000 kwa ajili ya kilimo Cha miwa na ujenzi wa kiwanda cha sukari na Rais wa awamu ya tano hayat.John Magufuli mnamo octoba mwaka 2017 ,Ili kuondokana na utegemezi wa kuagiza sukari nje ya nchi.