Rais wa Jamhuri Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye mazungumzo na Mwenyekiti wa Taasisi ya Wafanyabiashara ya Qatar Sheikh Faisal bin Qassim Al Thani aliyeambatana na ujumbe wa Wafanyabiashara wakubwa, Doha tarehe 06 Oktoba, 2022.
Rais wa Jamhuri Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye picha ya pamoja na Mwenyekiti wa Taasisi ya Wafanyabiashara ya Qatar Sheikh Faisal bin Qassim Al Thani aliyeambatana na ujumbe wa Wafanyabiashara wakubwa, Doha tarehe 06 Oktoba, 2022.
**********************
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ameshuhudia utiaji saini wa makubaliano ya ushirikiano kati ya Chemba ya Biashara ya Tanzania, Zanzibar na Chemba ya Biashara ya Qatar.
Kwa upande wa Chemba ya Biashara ya Tanzania, mkataba ulisainiwa na Rais wa Chemba hiyo Paul Koyi, huku pia ukisainiwa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kitaifa ya Wafanyabiashara Zanzibar (ZNCC) Ali Suleiman Amour.
Aidha, kwa upande wa Qatar mkataba huo umesainiwa na Makamu Mwenyekiti wa Chemba ya Biashara ya nchi hiyo Muhammed bin Ahmed Al Kuwari uliofanyika Jijini Doha.
Lengo la Mkataba huo ni kuimarisha Biashara na Uwekezaji kati ya wafanyabiashara wa Tanzania na Qatar hususan kwenye sekta za utalii, miundombinu, ujenzi wa mahoteli na usambazaji wa gesi.
Mbali na utiaji saini huo, Rais Samia amefanya mazungumzo na Waziri wa Fedha wa Qatar, Mhe. Ali bin Ahmed Al-Kuwari ambapo wamejadili masuala ya kikodi baina ya nchi hizo mbili, uwekezaji, biashara, gesi, ufugaji, utalii na kilimo.
Vilevile, katika mazungumzo ya Rais Samia na Waziri wa Afya wa Qatar, Mhe. Dkt. Hanan Mohamed Al Kuwari wamekubaliana wataalamu wa Tanzania wabadilishane uzoefu kwenye sekta ya afya hasa katika huduma za kibingwa na za dharura.
Rais Samia pia katika ziara yake ya kikazi alifanya mazungumzo na Amiri wa Qatar Sheikh Tamim bin Hamad al Thani, wafanyabiashara wakubwa na kuhudhuria Mkutano wa Ubunifu wa Afya Duniani (World Innovation Summit for Health) uliomalizika leo katika Kituo cha Elimu cha Multaqa Jijini Doha.