Na Mwandishi wetu, Babati
WANAFUNZI 17,238 wa darasa la saba wa Halmashauri ya ya Wilaya ya Mbulu, Mji wa Babati, Mji wa Mbulu na Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto Mkoani Manyara, wanafanya mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi.
Mkurugenzi wa halmashauri ya mji wa Mbulu, Yefred Myenzi amesema wanafunzi 3,193 wanatarajia kufanya mtihani huo kwenye eneo lake.
Myenzi amesema maandalizi yote yamefanyika ipasavyo hakuna chagamoto yoyote iliyojitokeza na amewatakia wanafunzi hao kila la heri kwenye mitihani yao.
“Matarajio yetu ni Mbulu mji kufanya vizuri kwenye upande wa taaluma kama tunavyofanya kwenye masuala mengine ya maendeleo,” amesema Myenzi.
Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Kiteto John John Nchimbi amesema wanafunzi 6,345 wanatarajia kufanya mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi.
Nchimbi amesema kati ya wanafunzi hao 6,348 wanaofanya mtihani wa kumaliza darasa la saba, wasichana ni 3,248 na wavulana wapo 3,100.
Hata hivyo, amesema kati ya wanafunzi hao 6, 348 wanaofanya mtihani wa kuhitimu darasa la saba mwaka huu, wanafunzi 6,474 ndiyo walioanza darasa la kwanza mwaka 2016.
“Hakuna changamoto yoyote iliyojitokeza kwenye shughuli ya ugawaji mitihani kila kitu kilikwenda kama kilivyopangwa nawatakia wanafunzi wote kila la heri kwenye mitihani yao,” amesema Nchimbi.
Kaimu Mkurugenzi wa mji wa Babati, Anna Fissoo amesema wanafunzi 2,816 wanaofanya mtihani kwenye eneo hilo wakiwemo wavulana 1,382 na wasichana 1,434.
Fissoo amesema mikondo ipo 126 na wasimamizi wa mikondo 126, wasimamizi wakuu 40 na akiba 10.
“Zipo shule 40 zinazofanya mtihani kati ya hizo 32 ni za shule za serikali na nane shule za binafsi,” amesema Fisoo.
Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu, Abubakari Kuuli amesema wanafunzi wanaofanya mtihani kwenye eneo hilo ni 4,884.
Kuuli amesema kati ya wanafunzi hao wanaofanya mtihani wavulana ni 2,164 na wasichana ni 2,720.