Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akiwa na Mwenyeji wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Maendeleo wa Abu Dhabi (Abu Dhabi Fund for Development), Mhe. Mohammed Saif Al Suwaidi, wakati walipokutana na kufanya mazungumzo kuhusu ushirikiano kati ya Tanzania na Mfuko huo, mjini Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akizungumza na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Maendeleo wa Abu Dhabi (Abu Dhabi Fund for Development), Mhe. Mohammed Saif Al Suwaidi, wakati walipokutana na kufanya mazungumzo kuhusu ushirikiano kati ya Tanzania na Mfuko huo, mjini Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akiwa katika picha na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Maendeleo wa Abu Dhabi (Abu Dhabi Fund for Development), Mhe. Mohammed Saif Al Suwaidi, wakati walipokutana na kufanya mazungumzo kuhusu ushirikiano kati ya Tanzania na Mfuko huo, mjini Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akiongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Maendeleo wa Abu Dhabi (Abu Dhabi Fund for Development), Mhe. Mohammed Saif Al Suwaidi, kuelekea kwenye eneo la mkutano baada ya kuwasili Ofisi za Makao Makuu ya Mfuo huo, mjini Abu Dhabi, Umoja wa Nchi za Falme za Kiarabu kwa ajili ya mazungumzo kuhusu ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na Mfuko huo.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (katikati), akiwa katika picha ya Pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Maendeleo wa Abu Dhabi (Abu Dhabi Fund for Development), Mhe. Mohammed Saif Al Suwaidi (wa tatu kulia), wakati walipokutana na kufanya mazungumzo kuhusu ushirikiano kati ya Tanzania na Mfuko huo, mjini Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu. Wengine ni Balozi wa Tanzania, Umoja wa Nchi za Falme za Kiarabu Mhe. Mohamed Mtonga (wa pili kushoto), Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango (Sera), Bw. Lawrence Mafuru (wa pili kulia), Kamishna Msaidizi Idara ya Sera, Wizara ya Fedha na Mipango Bw. William Mhoja (kushoto) na Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Abu Dhabi Fund Bw. Adel Abdulla Al Hosan (kulia)
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-WFM-Abu Dhabi)
………………………………..
Na Benny Mwaipaja, Abu Dhabi
Mfuko wa Maendeleo wa Abu Dhabi wa Umoja wa Falme za Kiarabu umeahidi kutoa mkopo nafuu kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo nchini Tanzania ukiwemo mradi wa umeme wa Benaco-Kyaka, mkoani Kagera na ujenzi wa makazi ya watumishi ya gharama nafuu Visiwani Zanzibar, inayokadiriwa kugharimu dola za Marekani milioni 420.
Ahadi hiyo imetolewa Mjini Abu Dhabi na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Maendeleo wa Abu Dhabi (Abu Dhabi Fund for Development), Mhe. Mohammed Saif Al Suwaidi, wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, Makao Makuu ya Mfuko huo, mjini Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu.
Mhe. Mohammed Saif Al Suwaidi alimweleza Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba kuwa miradi mingine ya kimkakati iliyowasilishwa na Serikali ya Tanzania kwenye Mfuko huo ukiwemo wa Ujenzi wa Bwawa la Kuzalisha Umeme la Julius Nyerere na Ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) itatafutiwa ufadili kupitia Serikali pamoja na Sekta Binafsi ya nchi hizo kwa kuwa inahitaji uwekezaji mkubwa wa fedha.
Aidha, Mkurugenzi Mkuu huyo wa Abu Dhabi Fund, Mhe. Suwaidi, alisema kuwa Mfuko wake uko tayari kusaidia pia utekelezaji wa miradi mingine ya kilimo na uvuvi na kwamba fedha hizo zitapatikana kupitia Kampuni inayojishughulisha na masuala hayo katika Serikali ya Umoja wa Falme za Kiarabu.
Akizungumza na mwenyeji wake, Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba alikumbushia upatikanaji wa fedha kwa ajili ya miradi sita iliyowasilishwa na Serikali ya Tanzania katika Mfuko huo ikiwemo mradi wa Ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kutoka Tabora-Kigoma-Msongati, Ujenzi wa Bwawa na Julius Nyerere, Mradi wa Umeme wa Benaco hadi Kyaka (220KV) mkoani Kagera, ujenzi wa nyumba 10,000 za makazi nafuu-Zanzibar, na mradi wa kuwezesha biashara ya usafirishaji na uingizaji wa bidhaa kutoka nje.
Aidha, Dkt. Nchemba, aliushukuru Mfuko huo kwa kutoa fedha kiasi cha shilingi mil. 201 na dola za Marekani milioni 1.3 kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa barabara ya Uvinza-Ilunde hadi Malagarasi yenye urefu wa kilometa 51.1 kwa kiwango cha lami, barabara ambayo ujenzi wake umerejea baada ya kukwama kwa muda mrefu.
“Maelekezo ya Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kwamba barabara hii ikamilike mapema ili kuleta manufaa ya kiuchumi na kijamii kwa pande zote mbili wakiwemo wananchi watakaoitumia barabara hiyo, na wabunge wa mkoa wa Kigoma wanaisubiri kwa hamu barabara hiyo” Alisema Dkt. Nchemba.
Dkt. Nchemba alimweleza Kiongozi huyo kuwa Tanzania imefungua milango kwa wawekezaji mbalimbali wakiwemo wanaotoka Abu Dhabi, kwenda kuwekeza Tanzania katika sekta mbalimbali ikiwemo ujenzi wa miradi ya kimkakati, kilimo, mifugo, uvuvi na ujenzi wa nyumba katika sekta za elimu, afya, kilimo na mifugo.
“Tumefurahi kwa kutuahidi kuwa miradi yetu mikubwa ya kimkakati ya kuzalisha umeme, reli ya kisasa, mmeichukua na kuipeleka Serikalini na kwenye sekta binafsi, tuo tayari kushirikiana nao na kwa upande wa kilimo na mifugo, nawahakikishia kuwa ardhi ipo ya kutosha” alieleza Dkt. Nchemba
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Lawrence Mafuru, alisema kuwa ahadi hiyo ni matunda ya kusainiwa kwa Mkataba wa kutotoza kodi mara mbili kwenye mapato ya faida pamoja na udhibiti wa ukwepaji kodi uliosainiwa juzi kati ya Tanzania na Umoja wa Falme za Kiarabu, mjini Dubai.
Alisema kuwa hatua hiyo itawezesha wawekezaji wengi zaidi wakiwemo wanaotoka katika sekta binafsi kwenda kuwekeza nchini Tanzania na kuleta faida za kiuchumi kwa nchi na wananchi kwa ujumla.
“wao kama Abu Dhabi Fund wanafadhili Sekta Binasfi ya hapa wanaowekeza katika nchi mbalimbali zikiwemo nchi za Afrika, kwa hatua tuliyoifanya ya kusaini makubaliano hayo ya kuondoa changamoto ya utozaji kodi mara mbili, tumefungua fursa nyingine kwa wawekezaji watakaokuwa wanawezeshwa na Mfuko huu kwenda kuwekeza nyumbani” Alisema Bw. Mafuru
Alisema kuwa Serikali inatekeleza mpango wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati na hivyo ni fursa ya kuvutia mitaji na uwekezaji kutoka ndani na nje ya nchi, wakiwemo wawekezaji kutoka Abu Dhabi ambao wameonesha nia ya kuwekeza kwenye kilimo, uvuvi, mifugo na maeneo mengine.
Mfuko wa Maendeleo wa Abu Dhabi umetoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali nchini Tanzania ukiwemo ujenzi wa Hospitali ya Wete-Pemba, barabara ya Kidawe hadi Uvinza (km 77), ujenzi wa Kiwanda cha Sukari cha Kagera na mradi wa maji Zanzibar vijijini ambayo imekamilika na hivi sasa wanafadhili ujenzi wa barabara ya Uvinza-Ilunde hadi Malagarasi wenye thamani ya dola za Marekani milioni 15.