Na Immaculate Makilika – MAELEZO
Waswahili husema “Alisifuye jua limemuangaza” naam na mie nianze kwa kusema tangu Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan iingine madarakani Machi 19, 2021 hadi sasa kumekuwepo na mapinduzi makubwa katika sekta mbalimbali ikiwemo utalii, uwezeshwaji wa wanawake na makundi maalum, uhusiano wa kidiplomasia, afya na biashara.
Licha ya maendeleo makubwa yaliyopatikana ndani ya muda mfupi, kumekuwa na mchango wa uhuru wa habari kwenye Serikali ya Awamu ya Sita katika ujenzi wa Tanzania ya Kidijitali ambao umeendelea kuboresha maisha ya Watanzania sambamba na kutoa fursa mbalimbali.
Tumeshuhudia uhuru maridhawa wa vyombo vya habari ambapo kupitia tamko alilolitoa Mhe. Rais Samia Aprili 6, 2021 la kuiagiza iliyokuwa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kuvifungulia vyombo vya habari na kuwataka watendaji waepuke kuvishughulikia kwa namna ambayo inaweza kusababisha Serikali kulaumiwa kwa kuminya uhuru wa habari.
“Wizara ya Habari, mnapaswa kusimamia vyombo vya habari, nasikia kuna vyombo vya habari huko mmevifungia, vifungulieni lakini vifuate sheria na kanuni”. Anasema Mhe. Rais Samia.
Agizo hilo la Rais Samia linadhihirisha namna ambavyo Serikali yake imedhamiria kujenga Tanzania ya Kidijitali, ambapo katika hotuba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye akiwasilisha bungeni Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha kwa 2022/23 anasema kuwa, Wizara yake ina jukumu la kutunga na kusimamia sera zinazohusiana na masuala ya Habari, Mawasiliano, na Teknolojia ya Habari kuratibu na kusimamia vyombo vya habari, na mawasiliano ya posta na simu.
Vilevile, kuendeleza wataalamu, tafiti na ubunifu kwenye masuala ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na kuendeleza na kusimamia miundombinu ya mawasiliano nchini ambapo utekelezaji wa majukumu hayo kutaiwezesha Tanzania kuimarika kushiriki uchumi wa kidijitali katika kufikia Mapinduzi ya Nne ya Viwanda (4th Industrial Revolution) yanayowezeshwa na kuendeshwa na TEHAMA na kuwa na jamii inayopata taarifa sahihi.
Hivyo basi, Serikali imeendelea kuweka miundombinu yenye kuruhusu ukuaji wa uhuru wa habari katika ujenzi wa Tanzania ya kidijitali.
“Agosti 19, 2021, Wizara ilifanikisha kusainiwa kwa mkataba kati ya Serikali na Benki ya Dunia wenye thamani ya dola za Marekani milioni 150 ambapo mradi ulianza kutekelezwa Novemba, 2021 na unalenga kuboresha na kukuza maunganisho ya ndani na ya kimataifa ili kuweza kufikisha huduma za mawasiliano pamoja na utoaji wa huduma mbalimbali za Serikali kwa wananchi. Vilevile, mradi huu unalenga kuboresha ubunifu pamoja na kuwajengea uwezo wataalam wa TEHAMA 500 kwenye maeneo ya ubobezi ili kujiandaa na uchumi wa kidijitali” Anasema Waziri Nape.
Pia, utekelezaji wa mradi huo umelenga kwenye kufanya maboresho ya sheria na miongozo kuwezesha kufikiwa kwa malengo ya Tanzania ya Kijiditali, kuunganisha taasisi 250 kwenye mtandao mmoja wa Serikali, kuanzisha vituo vya ubunifu kwa vijana, kuboresha mifumo ya TEHAMA na kuongeza uwezo kwenye Vituo vya Kutunzia data vya Taifa.
Aidha, Serikali imeendelea kuweka mazingira rafiki ya matumizi ya teknolojia za utangazaji hasa maudhui mtandaoni ambayo pia yamechangia kuongeza ajira kwa vijana. Ambapo redio, blogu na televisheni mtandao katika kipindi cha mwaka mmoja zimeongezeka kutoka televisheni mtandao 552 hadi 663 (ongezeko la 20.1%), blogu 134 hadi 148 (ongezeko la 10.4%), redio mtandao 25 hadi 27 (ongezeko la 8.0%) na majukwaa mtandaoni 9 hadi 10 (ongezeko la 11.1%).
Kumekuwa na ongezeko la vyombo vya utangazaji na kuwezesha kupanua wigo wa matangazo ya redio, televisheni na matangazo kupitia waya (Cable telivision). Redio zimeongezeka kutoka 119 hadi 210 (ongezeko la 76.5%), televisheni zimeongezeka kutoka 44 hadi 56 (ongezeko la 27.3%), matangazo kupitia waya kutoka 37 hadi kufikia 59 (ongezeko la 59.5%) na magazeti yameongezeka kutoka 270 hadi 284 (ongezeko la 5.2%).
Hayo yote yamewezesha kuongezeka kwa maudhui ya kibunifu kwa kuwepo kwa matumizi ya podcast na Watanzania kuwa na wigo mpana wa kutoa mawazo yao juu ya masuala mbalimbali huku mara kadhaa Mhe. Rais Samia akikumbusha “Tukosoeni kwa staha” na mie nashauri ni vyema tukaishi katika nyakati za utu na ustaarabu.
Fauka ya hayo, Tanzania iko tayari kuungana na dunia kutumia fursa zinazoletwa na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Ni dhahiri kuwa Mhe. Rais Samia ameimarisha uhuru wa habari na Tanzania ya kidijitali.