**************************************
NJOMBE
Wananchi mkoani Njombe wameitaka serikali kutoa adhabu ya kifungo kisichopungua miezi sita gerezani kama fundisho kwa wazazi na walezi ambao wanashirikiana na watuhumiwa wa mimba za wanafunzi pamoja na wale wanaowakatisha masomo watoto kwa kupeleka mijini kufanya kazi za ndani jambo ambalo linamkosesha mtoto haki ya msingi ya kupata elimu.
Mbali na kukatishwa ndoto ya kupata elimu imedaiwa kuwa watoto wengi pindi wanapotekeleza matakwa ya wazazi wao hujikuta kwenye wakati mgumu baada ya kuanza kupokea mateso na vipigo vikali kutoka kwa waajiri wao huko mijini.
Rai hiyo imetolewa na wazazi katika mahafali ya darasa la saba shule ya msingi Echo iliyopo mkoani Njombe akiwemo Jasinta Chama na Mohamed Buke ambaye ni Imamu wa msikiti wa mkoa huo ambapo wamesema katika miaka ya hivi karibuni kumekuwa na kesi nyingi za mimba mashuleni huku wengine wakidai kushinikizwa na wazazi wao kufanya vibaya katika mitihani ili wasiweze kufaulu kwa lengo la kupelekwa mijini kufanya kazi za ndani jambo ambalo limekuwa na athari kubwa kwa wanafunzi ikiwemo kupata mimba za utotoni na maisha ya tabu kila uchwao.
Wazazi hao wamesema ni vyema serikali ikatunga sheria ndogo za kuwabana hata wazazi ambao wanahusika katika kukwepesha ushahidi na kuamua kumalizana na watuhumiwa wa mimba za wanafunzi huku pia wakidai hata wale wanaokatisha masomo na kukimbizia mijini watoto wafungwe miezi sita ili kujifunza .
Wakati vitendo hivyo vinavyokiuka haki ya mtoto vikipingwa vikali katika baadhi ya jamii, nao baadhi ya wahitimu akiwemo Anitha Mlowe na Gerad Masasi wanasema wanafunzi wengi hukengeuka katika kipindi cha kusubiri majibu ya kujiunga na kidato cha kwanza hivyo ni vyema wazazi wakatumia kipindi hicho kuwapa masomo ya ziada pamoja na shughuli ndogondogo za nyumbani ili kuwaepusha na makundi mabaya.
Awali akizungumza mgeni rasmi katika mahafali hiyo Amini Mwakang’ata ambaye ni meneja wa benki ya CRDB tawi la Njombe amewaasa wazazi kuwapa urithi wa elimu watoto wao kwa maisha ya badae badala ya mashamba ili waweze kuja kuwasaidia uzeeni.
Aidha Mwakang’ata ametoa ushauri kwa wale wenye vipato duni ama uwezo mdogo wa kutunza fedha kufungua akaunti benki ili kutunza fedha za ada .
Takribani wanafunzi 15 wamehitimu na kukabidhiwa vyeti vya taaluma katika mahafali hiyo ya pili ya darasa la saba katika shule ya msingi Echo iliyopo halmashauri ya mji wa Njombe.