***************************
Na Mwandishi wetu, Mirerani
WACHIMBAJI wa madini ya ujenzi na viwandani wamepatiwa elimu na wataalam wa Tume ya Madini kupitia Mkoa wa kimadini wa Simanjiro.
Akizungumza kwa niaba ya Afisa Madini mkazi Mirerani, Nehemia Mudara amesema lengo lao ni kujadili hali halisi ilivyo, kwani Serikali inataka kuona mapato yake yanayotokana na madini ya ujenzi na viwandani yanaongezeka.
“Kwenye kikao chetu na wachimbaji wa madini ya ujenzi na viwandani tumeelezana vizuri na tumetoa elimu juu ya uchimbaji kuhusu kuzingatia mashine na ulipaji mirabaha ya Serikali kwa wakati,” amesema Mudara.
Amesema wamesisitiza ushirikiano kutoka kwao ili adhima ya Serikali ya
kuongeza mapato kupitia madini ya ujenzi na viwandaji iweze kufanyikiwa.
“Kikao chetu kimekuwa kizuri na wadau wetu kwani wamekuwa marafiki wa Tume ya Madini na tumefanikisha ushirikiano wa kutosha kati yetu,” anasema Mudara.
Mchimbaji na msafirishaji wa madini ya mchanga wa eneo la Losinyai, Emson Malonda amesema wamefaidika kupitia elimu waliyoipata ya kukusanya fedha kwa, kulipa mirabaha kwa wakati na upandishaji wa bei.
Malonda amesema hawawezi kubishana na Serikali kwani wanataka uchumi wa nchi upande kupitia asilimia zilizowekwa hivyo watashirikiana na Tume ya Madini kufanikisha hayo.
Mchimbaji mwingine wa madini ya mchanga, Loserian Soilei amesema elimu hiyo imewasaidia kuondokana na changamoto walizokuwa wanazipata ila kupitia ofisi ya Tume ya Madini wamepatiwa ufumbuzi.
Mchimbaji mwingine Edward Kefa amesema elimu waliyoipata ni nzuri
kwani pia wameelekezwa namna ya kutunza mazingira kwenye machimbo yao.