*******************************
NA MWAMVUA MWINYI,PWANI
KAMPENI ya chanjo ya magonjwa ya Surua Rubella kwa watoto wenye umri kati ya miezi tisa na chini ya miaka mitano , inatarajia kufikia watoto wapatao 165.875 Mkoani Pwani.
Pamoja na hilo, kampeni hiyo itahusisha utoaji wa chanjo ya polio ya sindano kwa watoto wapatao 93,546 wenye umri wa mwaka mmoja na nusu hadi miaka mitatu na nusu kwa ajili ya kujikinga na ugonjwa huo.
Mganga mkuu wa mkoa wa Pwani, dokta Gunini Kamba alieleza hayo ,wakati wa kikoa cha kamati ya afya ya msingi kwa ajili ya kampeni ya kitaifa ya chanjo ya Surua Rubella na Polio ya Sindano itakayoanza septemba 26 hadi septemba 30 huku uzinduzi ukitarajiwa kufanyika Chalinze.
“Lengo kuu la kitaifa ni kufikia zaidi ya asilimia 99 ya watoto waliolengwa kupata chanjo hizo ambapo mkoa umetenga timu 156 za uchanjaji ili kufikia vituo 553 na maeneo 245 ambayo ni magumu kufikika kutokana na sababu mbalimbali”alifafanua Gunini.
Aidha alielezea, kampeni hiyo inafadhiliwa na wadau wa shirika la GAVI ambao wametoa chanjo na fedha za utekelezaji kiasi cha shilingi milioni 251.9 kupitia shirika la afya duniani (WHO) pamoja na shirika la kuhudumia watoto duniani UNICEF .
Gunini alisema, hadi sasa mkoa umepokea na kusambaza chanjo katika halmashauri zote na usambazaji ngazi ya vituo unaendelea.
“Vile vile mkoa umepokea na kufunga majokofu yanayotumia nguvu ya umeme wa jua 33 katika halmashauri za Bagamoyo na Chalinze ikiwa ni awamu ya kwanza na awamu ya pili majokofu 115 kwa halmashauri zilizobaki mwishoni mwa mwaka huu”:
Akizindua kampeni hiyo, mkuu wa mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarist Ndikilo, alisema kiwango cha Surua Rubella kimeendelea kuwa juu ,kwa mkoa ni zaidi ya asilimia 100 idadi ya watoto wasiokamilisha chanjo na wasiochanjwa hali ambayo inaweza ikasababisha mlipuko wa ugonjwa wa surua.
“:Surua ni ugonjwa hatari na huathiri watu wa rika zote na dalili zake ni homa na vipele vidogo vidogo na ni chanzo kikuu cha maradhi,ulemavu, utapiamlo na vifo vya watoto wenye umri wa miaka mitano”
Ugonjwa wa Rubella dalili zake ni kama za Surua na madhara kwa mama mjamzito husababisha mimba kuharibika, au kuzaa mtoto mfu au njiti, ulemavu wa kimaumbile, yakiwemo matundu katika moyo, mtoto wa jicho, mtindio wa ubongo na makuzi hafifu.