Na Mwamvua Mwinyi, Kibaha
KATIBU Tawala mkoani Pwani ,(RAS )Zuwena Omary ameagiza kamati ya usimamizi ya ujenzi wa mradi wa nyumba ya watumishi wa zahanati ya Vikawe ,kata ya Pangani ,Kibaha unaofadhiliwa na mfuko wa Maendeleo ya jamii (TASAF),, ihakikishe inaongeza nguvu ya usimamizi ili mradi huo umalizike hadi itakapofika mwezi Novemba mwaka huu.
Ameeleza,mradi huo bado upo asilimia 70 na ulitakiwa uwe umekamilika mwezi uliopita.
Akitembelea ujenzi wa mradi wa soko la kisasa,machinjio ya kisasa,kituo cha afya Kidimu pamoja na ujenzi wa zahanati ya Mwanalugali ,Zuwena alieleza miradi haijakamilika kwa wakati kutokana na sababu mbalimbali hivyo watendaji wanapaswa kuwa na uchungu nayo ili ikamilike kwa wakati lengwa.
“Kuna miradi unakuta mkandarasi alikuwa hafiki eneo la mradi kutokana na changamoto ambazo nyingine ni za nyuma ,yaani mradi wa mwaka 2019 changamoto zinatajwa 2022,Naomba tusimame katika kufanya kazi na kutoa matokeo”alisisitiza Zuwena.
Hata hivyo alieleza ,Ujenzi wa nyumba za watumishi unasuasua , mradi uhakikishwe unaenda kasi .
Zuwena aliitaka Halmashauri, kamati simamizi kuongeza nguvu katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo na miradi ya TASAF kwa maslahi ya wananchi waweze kunufaika nayo haraka.
Mradi mwingine uliotembelewa ni ujenzi wa zahanati ya Mwanalugali ambao nao ulikwama kutokana na mfumo kufungwa lakini aliwahakikishia fedha inatoka mwishoni mwa mwezi huu septemba, na kuelekeza ikifika octoba 15 uwe umekamilika.
“Fanyeni kazi asubuhi ,mchana na usiku ili miradi ikamilike na kuhudumia wananchi ambao wanapata shida kufuata huduma mbali” Na Mimi kutembelea mradi kwa kushtukiza ni kawaida ,nitakuja wakati wowote kabla ya muda niliotoa ili kujiridhisha kama mradi unakwenda vizuri”alieleza Zuwena.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha, Mshamu Munde alisema wameamshwa , wanashukuru kwa maelekezo na wanaahidi kuyafanyia kazi mapungufu yaliopo na kutekeleza pale panapohitajika .
Ofisa TASAF mkoa wa Pwani Roseliwe Kimaro ,alizitaka TASAF Halmashauri,wilaya kushirikiana na maafisa mipango na kutoa taarifa za miradi na fedha kama ilivyo taratibu zinavyofanywa kwenye miradi mingine ya Serikali .
“Serikali ni moja , wote ni kitu kimoja , ushirikiano uwepo ili kuwa na taarifa moja ya utekelezaji”alisema Roseliwe.
Ofisa mipango mji wa Kibaha Wambura Yamo alielezea, mradi wa ujenzi wa nyumba ya watumishi Zahanati ya Vikawe unashirikisha mitaa miwili ya Vikawe Bondeni na Vikawe Shule.
Wambura alibainisha, mradi huo ni wa sh.milioni 104.660,785.7 kati ya fedha hizo gharama ya vifaa na ufundi sh.91.964.285.7.
Mradi wa ujenzi wa zahanati ya Mwanalugali A ,unagharimu sh.113.964.285.7, kati ya fedha hizo gharama ya vifaa na ufundi ni sh.91.964.285.7 na mchango wa jamii ni sh.milioni 22.