Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi imekuwa ikipokea malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusu kucheleweshwa kupatiwa hati, hata baada ya kukamilisha taratibu zinazokidhi vigezo.
Kufuatia hali hiyo, Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi ameelekeza Ofisi zote za Ardhi za Mikoa kuhakikisha zinakamilisha zoezi la utoaji hati kwa zile hati ambazo taratibu zake zimekamilika ndani ya mwezi mmoja kuanzia tarehe ya tangazo hili. Aidha, kama kuna kikwazo chochote cha utoaji hati kwa sababu yoyote ile, wahusika watapewa taarifa ya maandishi ya sababu ya hati kuchelewa na kushauriwa hatua za kuchukua ili taratibu zikamilishwe.
Pamoja na taarifa hii, Wizara ya Ardhi inapenda kuufahamisha umma kuwa, ofisi zote za Ardhi za Mikoa zimeanzisha utaratibu wa kutoa huduma jumuishi za utoaji hati (One Stop Office) kwa lengo la kurahisisha upatikanaji Hatimiliki za Ardhi.Utaratibu huu unalenga kuondoa usumbufu wa kufuatilia taarifa za kukamilisha hatua mbalimbali za kisheria kabla ya kupata hati.
Wizara pia inapenda kuwafahamisha wamiliki wote wa ardhi kuwa, inazo takriban Hati 20,000 zilizokamilika lakini wahusika hawajazichukua. Wito unatolewa kwa wahusika wote kufika ofisi za Ardhi za mikoa kuchukua hati zao.
Orodha za Hatimiliki ambazo hazijachukuliwa zimebandikwa katika mbao za matangazo za Ofisi za Ardhi za Mikoa na Halmashauri nchini.
Aidha, Wizara ya Ardhi inamtaka mwananchi yeyote mwenye malalamiko ama changamoto kuhusu utoaji huduma za sekta ya ardhi kwenye ofisi zetu kupiga simu Kituo chetu cha Huduma kwa Wateja kupitia simu 0739646885 au 026216110 kwa ajili ya kuwasilisha kero yake.
IMETOLEWA NA KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI