NA MWAMVUA MWINYI,KIBAHA
MTU mmoja amefariki dunia na wengine wawili kujeruhiwa na chuma chakavu kidhaniwacho ni bomu ambacho kilisababisha mlipuko mkubwa huko Msangani ,Kibaha mkoani Pwani .
Aidha Jeshi la polisi kwa kushirikiana na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ )imeokota vipande vitano vya chuma chakavu vidhaniwayo ni mabomu katika eneo hilo la tukio na kuendelea na uchunguzi.
Kamanda wa polisi mkoani hapo,Wankyo Nyigesa akithibitisha juu ya tukio hilo alisema , septemba 20 kitu kama chuma kidhaniwacho ni bomu kililipuka na kumjeruhi na hatimae kumsababishia kifo cha Mbaraka Kolomela 37,mkazi wa Msangani,mnunuzi wa vyuma chakavu.
Alieleza, marehemu alifika nyumbani kwa Rajabu Nyangare (50) mkazi wa Msangani muuzaji wa vyuma chakavu kwa lengo la kununua vyuma chakavu.
“Wakati marehemu anafanya uchambuzi wa vyuma hivyo kuvitoa upande mwingine ndani wa jengo ambalo halijakamilika mali ya Rajabu Nyangare ndipo ulitokea mlipuko mkubwa uliosababisha majereha na kifo”
Wankyo alisema watu wawili waliojeruhiwa walikuwa karibu na eneo la tukio .
Aliwataja waliojeruhiwa kuwa ni, Fatuma Likupila (61) ambae alijeruhiwa kichwani na masikio na mlipuko huo,alitibiwa Tumbi na sasa amekimbizwa hospital ya Taifa ,kwani hali yake ni mbaya.
Mwingine ni Shomari Athumani (26) aliyepata jeraha pajani na tumboni amelazwa Tumbi kwa matibabu zaidi.
Alibainisha ,wanamsaka mmiliki wa vyuma chakavu Rajabu Nyangare,mkazi wa Msangani ambae alitoroka baada ua mlipuko huo kutokea ili achunguzwe uhalali wa leseni yake ya ununuzi wa vyuma chakavu na mlipuko ambao ulitokea baada ya marehemu kwenda kununua vyuma hivyo kwa mmiliki huyo.
Alitoa wito ,kwa wananchi kuacha tabia ya kuokota vyuma na kuhifadhi majumbani bila tahadhali.