Asila Twaha, TAMISEMI
Serikali imesema kuwa, itaendelea kuboresha miundombinu ya elimu katika ujifunzaji na ufundishaji kwa kuhakikisha Mafunzo Endelevu ya Walimu Kazini (MEWAKA) yanafikia lengo.
Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Dkt. Grace Magembe anayeshughulikia afya amebainisha hayo Septemba 19, 2022 Jijini Dodoma wakati akifungua Mafunzo Endelevu ya Walimu Kazini (MEWAKA) kwa wawezeshaji wa Kitaifa lengo likiwa kuwajengea uwezo wakati watakapokwenda kutekeleza majukumu yao katika ngazi ya Mikoa na Halmashauri.
Ameeleza kuwa Serikali imeendelea kuboresha vituo vya walimu (TRCs) vitakavyotumika kutoa Mafunzo endelevu ya Walimu Kazini pamoja na kununua vifaa vya TEHAMA vitakavyosaidia katika uendeleshaji wa mafunzo hayo.
“Mafunzo haya yamepangwa kutolewa katika ngazi za shule na vituo vya walimu ambapo walimu wote wanaelekezwa kushiriki kikamilifu” amesisitiza Dkt. Grace
Mafunzo hayo yamelenga kufikia Halmashauari 40 ambazo hazijapatiwa mafunzo.
Aidha, Dkt. Grace amesema Halmashauri 19 kati 40 zilizobaki katika Mikoa ya Kigoma, Tanga, Simiyu, Mara, Rukwa, Singida na Dodoma zitapatiwa mafunzo kwa walimu wa shule ya msingi kupitia programu ya Shule Bora.
Amewataka viongozi wanaosimamia mpango huo na wawezeshwaji kusimamia kikamilifu mpango huo ambao Serikali kwa kushirikiana na wadau wameuwekeza.
Amewataka kuhakikisha kuwa, mafunzo hayo yanakuwa na tija na endelevu kwa walimu.
Pia, amewaagiza walimu wote nchini kushiriki kikamilifu mafunzo hayo katika jumuiya za kujifunza kwa ngazi ya shule na vituo vya walimu.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET)Dkt. Aneth Komba ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuwawezesha walimu kwa kuwapatia mfunzo na kueleza kuwa, mafunzo hayo yatatoa nafasi ya walimu kuweza kupata mbinu tofauti za kufundishia na kuweza kuwaelekeza jinsi ya kuweza kusoma kwa maktaba mtandao lakini pia kuweza kutumia njia ya “Learning Management System (LMS) ambayo itawawezesha kupata nyenzo tofauti za kufundishia kwa kutumia njia ya kieletroniki.
Mwenyekiti wa Mafunzo Endelevu ya Walimu Kazini Bi. Modesta Ng’aida(Mkufunzi chuo cha Ualimu Butimba) kwa niaba ya wawezeshwaji hao amesema, mafunzo hayo watakayopata yatakuwa ni mwongozo wa kuwawezesha kwenda kuwa mabalozi wazuri katika maeneo watakao elekezwa kuenda kuyatekeleza.
“Tunaihakikishia Serikali yetu hamjakosea sisi tunaowakilisha wenzetu tutahahakikisha tunaifikisha elimu tuliyoipata kwa manufaa ya watoto wetu ambao ndio wanafunzi wetu” amesema Ng’aida
Pia, Dkt. Grace amtoa wito kwa walimu kuendelea kutoa elimu ya shuleni na duniani kwa kujua kuwa wao wamepewa jukumu kubwa la kuaminika.
“Walimu mnajukumu kubwa sana tusaidianeni na wazazi ili kuwasimamia watoto kwa kuwaongoza katika elimu ya shule na duniani ili watoto wetu wawe ni wenye tabia njema”
amesema Dkt. Grace