Na Dotto Mwaibale, Singida
WATU wawili wamefariki dunia baada ya magari aina ya Noah waliokuwa wakisafiria kugongana uso kwa uso eneo la Utaho Barabara Kuu ya kutoka Dodoma kwenda Singida wilayani Ikungi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Stellah Mutabihirwa amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo iliyotokea leo Septemba 18, 2022 majira ya mchana katika eneo hilo.
Mutabihirwa alisema watu waliopoteza maisha katika ajali hiyo ni wanaume akiwepo Katibu wa Msikiti wa Kati (BAKWATA) mjini hapa aliyefahamika kwa jina la Hamisi Dinya ambaye alikuwa akienda kumpokea Mufti wa Tanzania Sheikh Dk. Abubakar Zuberi Bin Ally wa Mbwana ambaye ameanza leo ziara yake ya kikazi ya siku mbili mkoani hapa pamoja na mtoto mmoja ambaye jina lake halijafahamika.
Alisema majeruhi katika ajali hiyo ni saba na kuwa walikimbizwa Hospitali ya Misheni ya Puma kwa ajili ya matibabu na kuwa hali ya majeruhi mmoja ni mbaya.
Kamanda Mutabihirwa alisema chanzo cha ajali hiyo ni moja ya magari hayo lililokuwa likitokea Ikungi kuelekea Singida mjini dereva wake kuwa katika mwendo mkali huku akijaribu kuyapita magari mawili kwa mpigo hivyo kushindwa kulimudu na kusababisha ajali hiyo.