Na John Walter-Babati
Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mjini Babati (BAWASA) imejiandaa kuwalipa fidia wakazi 25 wa Maisaka A wanaoishi kwenye maeneo ambayo serikali imeyaandaa kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya maji.
Akizungumza na wananchi hao mkuu wa wilaya ya Babati Lazaro Twange amesema zoezi hilo litakuwa wazi na hakuna atakayeonewa.
Meneja ufundi wa Mamlaka ya maji safi na usafi wa Mazingira mjini Babati (BAWASA) Honolath Sebastian amesema wamepitia maeneo yote ambayo yanapaswa kulipwa fidia na kuyaorodhesha likiwemo eneo la nyumba ya ibada (MSIKITI) na kwamba watafuata taratibu zote za kisheria katika kuwahamisha.
Mthamini wa Mkoa wa Manyara Pius Oswin amewaambia wakazi hao kwamba zoezi litaanza Jumatatu kwa kutolewa fomu namba 26 kwa ajili ya tathmini kwa wote wanaohusika.
Wananchi hao wamesema walikuwa wakiishi kwa hofu wakidhani kuwa wangehamishwa kwa nguvu katika maeneo yao bila fidia na kwamba baada ya mkuu wa wilaya kuzungumza nao wapo tayari kupisha.
Hata hivyo wananchi hao wameiomba BAWASA waharakishe mchakato wa kuwalipa fidia ya kuhama ili wasiendelee kufanya shughuli za kibinadamu katika maeneo hayo.