Na Mwandishi wetu, Arusha
VIONGOZI wa kimila wa jamii ya masai, Barbeig, Akie na wataturu wamesaini makubaliano ya kukubali kushiriki katika mradi wa bomba la mafuta kutoka Hoima Uganda hadi Tanga.
Viongozi hao wamesaini makubaliano na kampuni ya ujenzi wa bomba la mafuta ya EACOP Tanzania hafla iliyofanyika Mount Meru hoteli na kuhudhuriwa na viongozi wa serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali ambayo yanafanyakazi na jamii hizo.
Akizungumza kwa niaba ya wazee wa mila Laigwanani Joseph Laizer amesema wamekubali kuwa na makubaliano na kampuni ya EACOP baada ya kuwashirikisha katika mradi huo.
“Sisi kama viongozi tumeridhishwa na makubaliano ya leo na tutakwenda kuwa mabalozi kwa wengine” amesema.
Hata hivyo kiongozi huyo ameitaka kampuni ya EACOP kutekeleza yote walioyokubaliana.
Mkurugenzi wa kampuni ya EACOP Tanzania, Wendy Brown amesema watatekeleza yote waliyoahidi na watashirikiana katika mpango kazi wa mradi wa bomba la mafuta na watahakikisha wananufaika.
Amesema watawashirikisha katika utekelezaji wa mradi, kuzijengea uwezo jamii hizo katika masuala ya kiuchumi, kuzisaidia kupata huduma muhimu kama elimu na afya, kuendeleza masuala ya utamaduni.
Afisa Nishati kutoka Wizara ya Nishati, Yovin Uisso amesema serikali itahakikisha makubaliano yaliyofikiwa baina ya EACOP na jamii hizo yatatekelezwa na pande zote.
Amesema katika kuhakikisha jamii hizo zinanufaika na mradi huo serikali itatoa fursa ya upendeleo kwa baadhi ya vitu ikiwepo ajira.
Mshauri elekezi wa mradi huo, katika masuala ya haki za binaadamu, Dkt Elifuraha Laltaika, amesema kampuni EACOP imesaini makubaliano na jamii hizo ikiwa ni kuheshimu sheria na vigezo vya kimataifa zinazolinda haki za jamii za pembezoni.
Amesema masuala ya haki za jamii hizo yamezingatiwa katika mradi huo.
Viongozi waliosaini makubaliano hayo ni kutoka wilaya za Simanjiro, Kiteto, Kilindi, Handeni, Igunga, Kondoa na Hanang’.