Na Lilian Lundo – MAELEZO, Arusha
Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa amewataka Watanzania kulinda miundombinu ya majitaka iliyojengwa kwa gharama kubwa na Serikali.
Msigwa amesema hayo jana, Septemba 13, 2022 alipotembelea mradi wa mabwawa ya kutibu majitaka unaosimamiwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Arusha (AUWSA).
“Watanzania tuna wajibu wa kushiriki katika utunzaji wa miundombinu ya majitaka. Moja ya changamoto tulizoziona katika mabwawa haya ni kuwepo kwa taka ngumu ambazo zinawekwa kwenye mfumo wa majitaka, ambapo tumeona nguo, vipande vya makarai na vipande vya masufuria, jambo ambalo si sahihi,” alifafanua Msigwa.
Aliendelea kusema kuwa, wakazi wa Arusha na miji mingine yenye miradi kama hiyo kuhakikisha matumizi mazuri ya miundombinu ya majitaka yanazingatiwa, kwa kuilinda ili isiharibiwe na kuitumia kwa usahihi.
“Haipendezi ukachukua suruali yako ya jinzi ukaiweka kwenye mfumo wa majitaka, kitakachotokea mfumo utaziba, na mfumo ukiziba huduma itasimama. Huduma ikisimama sisi wenyewe tunakuwa tumejiadhibu badala ya kunufaika na huduma tuliyowekewa,” alifafanua Msigwa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji AUWSA, Mhandisi Justine Rujomba amewataka wakazi wa Jiji la Arusha kutunza miundombini ya majitaka ambayo imegharimu Serikali fedha nyingi.
“Tutumie miundombinu ya majitaka vile inavyostahili, kwa sasa tunapata changamoto kubwa mtandao unaziba, lakini ukienda kuzibua utakuta nguo na makopo,” alisema Mhandisi Rujomba.
Hivyo, amewataka Wananchi wa Jiji la Arusha kushirikiana na AUWSA kutoa taarifa ya uhalibifu wowote wa miundombinu unapotokea katika maeneo yao.
Mradi wa mabwawa ya kutibu majitaka umegharimu Shilingi bilioni 15 ambao una uwezo wa kutibu majitaka lita milioni 22 kwa siku, na mpaka sasa jumla ya wateja 4,000 wameunganishwa na mfumo huo.