*******************
KAMPENI MAALUM YA KUSALIMISHA SILAHA HARAMU.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linapenda kuwataarifu wananchi wote kuwa kuanzia tarehe 01/09/2022 hadi tarehe 31/10/2022 ni kampeni maalum ya usalimishaji wa silaha haramu kwa hiari zinazomilikiwa na watu kinyume cha sheria, ama kwa kutokujua taratibu za kisheria za umiliki halali wa silaha.
Mapema Septemba 05, 2022 Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe.Jumanne Sagini alizindua rasmi kampeni hiyo Jijini Dodoma ambayo itadumu kwa muda wa miezi miwili.
Kwa mwanamchi yeyote ambaye anamiliki silaha kinyume cha sheria anapaswa kusalimisha silaha hiyo/hizo kwa hiari katika ofisi za serikali ngazi ya Mtaa au Kijiji kuanzia saa 02:00 asubuhi hadi saa 10:00 jioni. Pia anaweza kusalimisha silaha kituo chochote cha Polisi kilicho jirani/karibu naye. Kwa mwanachi yeyote atakaye salimisha silaha kwa hiari ndani ya muda uliotangazwa, hatochukuliwa hatua zozote za kisheria.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linatoa rai kwa wananchi kushiriki kampeni hii kwa kuhakikisha wanasalimisha silaha kwa hiari katika maeneo tajwa hapo juu. Aidha ni rai kwa wananchi kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi pindi wasikiapo tangazo hili kwa kuwajulisha wananchi wengine ili kuepuka mkono wa sheria kwa kisingizio cha kutosikia tangazo hili mara muda uliotolewa na Mhe.Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi kupita.
Mara baada ya kampeni hii kumalizika, Jeshi la Polisi litafanya operesheni maalum kichwa kwa kichwa, nyumba kwa nyumba, mtaa kwa mtaa ili kuwabaini na kuwachukulia hatua za kisheria wale watakaobainika kukaidi kampeni hii na kuendelea kumiliki silaha kinyume cha sheria. “SILAHA HARAMU SASA BASI, SALIMISHA KWA HIARI”
MTANDAO WA WIZI WA MAGARI WATIWA MBARONI MBEYA.
Mnamo tarehe 04/04/2022 majira ya saa 02:00 usiku huko Mtaa wa Jelele, Kata ya Itezi, Tarafa ya Sisimba, Jijini Mbeya. Afisa Kilimo Wilaya ya Mbeya Vijijini GIDION MAPUNDA [45] aliibiwa Gari lake lenye namba za usajili T.795 DEX aina ya Prado TX rangi ya Silver na mtu/watu wasiofahamika.
Kufuatia tukio hilo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya lilianza kufanya ufuatiliaji wa tukio hilo na mnamo tarehe 05/07/2022 tulifanikiwa kuwakamata watuhumiwa watatu kuhusiana na tukio hilo ambao ni:-
- YUSUPH OMARY RAMADHANI [26] Mkazi wa Forest Jijini Mbeya.
- SHUKU JOSEPH NYEMA [23] Mkazi wa Songea Mkoa wa Ruvuma.
- ABUU NOELY RUTAGALAMA [26] Mkazi wa Itezi Jijini Mbeya.
Katika mahojiano, watuhumiwa walikiri kuhusika katika tukio hilo na kudai kuwa Gari hilo wamelisafirisha hadi nchi jirani ya Malawi na kumkabidhi mtu aitwaye RICHARD NG’OMA @ PINDA [35] raia wa nchini Malawi.
Kupitia ushirikiano wa ujirani mwema, mnamo tarehe 31/08/2022 hadi 02/09/2022 Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya lilifika mpaka nchini Malawi na kushirikiana na Polisi Malawi ambao walifanya ufuatiliaji na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa RICHARD NG’OMA @ PINDA akiwa na Gari hilo na kukiri kulipokea kutoka kwa mtuhumiwa YUSUPH OMARY.
Mnamo tarehe 02/09/2022 mtuhumiwa RICHARD NG’OMA @ PINDA alifikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kalonga nchini Malawi na kutolewa ushahidi na mmiliki wa Gari hilo GIDION MAPUNDA [45] na mtuhumiwa YUSUPH OMARY [26] ambapo baada ya mahakama kujiridhisha na Ushahidi uliotolewa ilimtia hatiani mtuhumiwa na kukabidhi Gari hilo kwa Jeshi la Polisi Tanzania kwa ajili ya taratibu za kumrejeshea mmiliki halali.
ATIWA MBARONI KWA KUPATIKANA NA MAGUNIA YA BHANGI.
Mnamo tarehe 05/09/2022 majira ya saa 11:00 jioni huko Kitongoji cha Chikula, Kijiji na Kata ya Ifumbo, Tarafa ya Kiwanja, Wilaya ya Chunya, Mkoa wa Mbeya. Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya lilifanya msako na kufanikiwa kumkamata MABULA MABHEMBE @ MALE [35] Mkazi wa Chikula akiwa anauza dawa za kulevya aina ya Bhangi katika duka lake la bidhaa za nyumbani.
Katika upekuzi uliofanywa na Jeshi la Polisi kwa mujibu wa sheria, mtuhumiwa alikutwa na bhangi magania matatu yenye uzito wa kilogramu 20, misokoto 3,500 pamoja na rizla boksi 02 ndani ya duka lake la biashara ya bidhaa za nyumbani.
Mtuhumiwa amehojiwa na kukiri kufanya biashara ya kuuza dawa hizo za kulevya kwa kushirikiana na mtuhumiwa mwingine aitwaye HAMIS SHAURITANGA ambaye anaendelea kutafutwa na Jeshi la Polisi. Upelelezi unaendelea na mara baada ya kukamilika mtuhumiwa atafikishwa mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria.
Aidha ninamtaka mtuhumiwa mwingine popote alipo ajisalimishe kituo cha Polisi. Pia nitoe rai kwa wananchi kwa yeyote mwenye taarifa za mahali alipo mtuhumiwa asisite kuzitoa kwa Jeshi la Polisi ili akamatwe na kutendewa kwa mujibu wa sheria. Niwatake wananchi na wakazi wa Mbeya kufanya biashara halali kwa ustawi wa uchumi na maendeleo ya mtu mmoja mmoja, familia zetu, mkoa wetu na taifa kwa ujumla kwani biashara haramu kwa Mbeya hazilipi na watafilisika bure.
MWANAFUNZI WA KIDATO CHA TANO ATIWA MBARONI KWA TUHUMA ZA MAUAJI.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia mwanafunzi wa kidato cha tano katika Shule ya Sekondari Iduda aitwaye HUMPHREY HUMPHREY @ NGOGO [17] kwa tuhuma za mauaji ya mwanafunzi mwenzake mtoto wa kike aitwaye FARAJA KASOLE [16] Mwanafunzi wa Kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Sinde
Ni kwamba mnamo tarehe 02.09.2022 majira ya saa 10:45 jioni huko Mtaa wa Mkuyu, Kata ya Iganzo, Tarafa ya Iyunga, Jijini Mbeya. Mtoto wa kike aitwaye FARAJA KASOLE [16] Mwanafunzi wa Kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Sinde aliuawa kwa kupigwa na shoka kichwani na mtuhumiwa.
Chanzo cha tukio hili ni tamaa za kimwili ambapo mtuhumiwa alijaribu kumbaka marehemu lakini baada ya kuzidiwa nguvu ndipo alichukua shoka na kumpiga nalo kichwani.
Kabla ya tukio hilo, mtuhumiwa alifika nyumbani kwa marehemu ambaye kwa muda huo alikuwa peke yake na kisha kumvamia chumbani kwake kwa nia ya kumbaka na alipozidiwa nguvu ndipo aliamua kuchukua shoka na kumpiga nalo.
Mtuhumiwa amekamatwa, upelelezi wa shauri hili unaendelea na mara baada ya kukamilika atafikishwa mahakamani.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linalaani tukio hili baya kutokea na linatoa pole kwa wazazi na familia ya marehemu. Aidha ninaendelea kutoa rai kwa wazazi na walezi kujenga tabia ya kuzungumza na watoto wao na kuwataka kujikita zaidi kwenye masomo na kuachana na tamaa za kimapenzi wangali masomoni ili kuepuka matukio kama haya.