WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Innocent Bashungwa,akizungumza wakati akifungua Mkutano wa mwaka wa 85 wa Chama cha Madaktari wa Kikristu Tanzania (TCMA) leo Septemba 5,2022 jijini Dodoma.
Rais wa Chama cha Madaktari wa Kikristu (TCMA) Dk.Paul Kisanga,akisoma risali wakati wa Mkutano wa mwaka wa 85 wa Chama cha Madaktari wa Kikristu Tanzania (TCMA) leo Septemba 5,2022 jijini Dodoma.
Mkurugenzi wa Mtendaji wa shirika la Christian Social Services Commission (CSSC), Peter Maduki ,akitoa neno la shukrani amemhakikishia Waziri Bashungwa kuendelea kufanya kazi na serikali kwa ushirikiano mkubwa wakati wa Mkutano wa mwaka wa 85 wa Chama cha Madaktari wa Kikristu Tanzania (TCMA) leo Septemba 5,2022 jijini Dodoma.
SEHEMU ya Washiriki wakifatilia hotuba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Innocent Bashungwa (hayupo pichani),wakati akifungua Mkutano wa mwaka wa 85 wa Chama cha Madaktari wa Kikristu Tanzania (TCMA) leo Septemba 5,2022 jijini Dodoma.
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Innocent Bashungwa,akiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kufungua Mkutano wa mwaka wa 85 wa Chama cha Madaktari wa Kikristu Tanzania (TCMA) leo Septemba 5,2022 jijini Dodoma.
………………………………………
Na Alex Sonna-DODOMA
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Innocent Bashungwa ,amezindua mkutano wa mwaka wa 85 wa Chama cha Madaktari wa Kikristu Tanzania (TCMA).
Akizindua mkutano huo leo Septemba 5,2022 jijini Dodoma Bashungwa amesema hataki kusikia kuna mawasiliano na mahusiano hafifu kati ya waganga wakuu wa mikoa,wakurugenzi wa halmashauri na taasisi za Dini ambazo zinatoa huduma za afya kwa wananchi.
Kauli hiyo imekuja kufuatia Rais wa Chama cha Madaktari wa Kikristu (TCMA) Dk.Paul Kisanga, kueleza katika risala moja ya changamoto wanazokutana nazo ni kuwa baadhi ya halmashauri zimekuwa zikishindwa kuhuisha mikataba ya vituo vya afya vya kanisa hata pale ambapo bado kituo cha serikali hakijafikia kutoa huduma stahiki kwa wagonjwa.
Waziri Bashungwa amesema suala la mahusiano kati ya serikali na taasisi za dini ambazo zinatoa huduma za afya kwa wananchi ni muhimu.
Waziri Bashungwa amemwagiza Katibu Mkuu wa Tamisemi, Profesa Riziki Shemdoe kuweka mikakati ya kuboresha mahusiano kati ya waganga Wakuu wa Mikoa,Wakurugenzi na taasisi za dini ambazo zinatoa huduma kwa wananchi.
“Lakini ni lazima tuboreshe patnership mimi Waziri wa Nchi Tamisemi kwakuheshimu majukumu ambayo TCMA mnayafanya kwa kushirikiana na Serikali nimeacha majukumu ili kuangalia jambo linaenda vizuri.
“Immediately tuanzie hapo lakini sasa tuipe timu mapitio hayo ya mikataba waipitishe ili tukubaliane jinsi ya kulitekeleza,” amesema Waziri Bashungwa.
Waziri Bashungwa amesema Serikali imekuwa ikifanya juhudi katika kuboresha sekta ya afya kwa kushirikiana na taasisi za dini ambapo katika kipindi cha mwaka 2021-2022 imetumia zaidi ya Sh 383 bilioni kwa ajili ya zahanati 564 vituo vya afya 304 na hospitali za Wilaya 68.
“Sasa tukichukua takwimu hizi na kwenye upande wa taasisi za dini rais wenu ametaja takwimu na mikataba ambayo tunajadili na kuhuisha itaenda kuboresha vituo vya tiba.
Waziri huyo amesema Sh 103.09 bilioni zimetumika kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba kwenye zahanati vituo vya afya na hospitali za Wilaya.
Amesema mwaka huu wa fedha Serikali imetenga jumla ya Sh 69.9 bilioni kwa ajili ya kuendelea kununua vifaa tiba.
“Jitihada kubwa zimekuwa zikifanyika katika kujenga miundombinu lakini bado tuna pengo ambalo tunaendelea kulijaza.
“Nitumie nafasi hii kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan hivi tunavyozungumza tumeishafanya na kukamilisha mikataba tupo katika hatua za manunuzi ya kununua vifaa tiba ikiwemo magari vyenye thamani ya shilingi bilioni 149.5,”amesema Bashungwa
Kuhusu changamoto ya ajira,Waziri Bashungwa amesema wataendelea kulitatua kwa kushirikiana na taasisi hizo za dini.
Awali,Rais wa Chama cha Madaktari wa Kikristu (TCMA) Dk.Paul Kisanga, amesema kuwa lengo la mkutano huo ni kujadili jinsi ya kuendeleza hospitali za taasisi za dini, kuboresha huduma za afya na kukuza ushirikiano kati ya madaktari na watoa huduma pamoja na kubadilishana mawazo kutafuta njia za kutatua matatizo ya utoaji wa huduma.
“Mada kuu ni kila mwaka inachaguliwa mada maalum inayolengwa kwenye shabaha na kwa mwaka huu tumelenga kwenye maboresho ya hospitali za kanisa katika utoaji wa huduma za afya na upatikanaji wa rasiliamli fedha endelevu,”amesema Dk.Kisanga
Amesema Hospitali nyingi za makanisa zipo katika maeneo ya vijijini ambako ndiko walipo wananchi wengi na watu wenye uwezo mdogo wa kumudu hali ya maisha.
“Tunafahamu Serikali inavyothamini mchango wa kanisa hadi mwanzoni mwa mwaka huu kanisa kwa pamoja limeendesha vituo zaidi ya 900 vya huduma za afya ikiwemo hospitali 105 ikiwemo tano za Rufaa ngazi ya kanda.
Amesema hospitali 12 zikiwa na huduma za rufaa ngazi ya Mkoa na 37 ni zinatumika kama hospitali za wilaya na kuzifanya hospitali teule
Amesema wana vituo vya afya 134 kati ya hivyo kuna ambavyo vinalaza wagonjwa wengi kuliko hata hospitali kutokana na mahitaji makubwa
Amesema wanaipongeza Serikali na Tamisemi kwa kuendelea kuboresha sekta ya afya na wanauhakika huduma za afya hata zile za kibingwa zitaendelea kuongezeka.
Naye Mkurugenzi wa Mtendaji wa shirika la Christian Social Services Commission (CSSC), Peter Maduki akitoa neno la shukrani alimhakikishia Waziri Bashungwa kuendelea kufanya kazi na serikali.
“Mheshimiwa Waziri nikuhakikishie tupo tayari kufanya kazi na Serikali na kuhakikisha malengo ya serikali ya Raisi wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania inafikiwa sisi tunakuhakikishia yote yatafanyika.Na tutakuwa na mikutano kila robo mwaka kwa ajili ya kujadiliana maendeleo na changamoto mbalimbali,” amesema.
Shirika la Christian Social Services Commission (CSSC) linaratibu na kusimamia utolewaji wa huduma za afya kwenye vituo vya afya vipatavyo 900 na huduma za elimu kwenye taasisi za elimu zaidi ya 1000 zinazomilikiwa na taasisi za dini nchini Tanzania.