Na Kassim Nyaki, Handeni.
Kamati ya kudumu ya Bunge ya ardhi, maliasili na utalii leo tarehe 3 Septemba, 2022 imefanya ziara katika Kijiji cha Msomera Handeni Mkoani Tanga kwa lengo la kukagua ujenzi wa nyumba za makazi, huduma za kijamii, miundombinu na hali ya maisha ya wananchi kutoka Ngorongoro waliohama kwa hiari Kijiji hapo.
Kamati hiyo iliyoongozwa na mwenyekiti wake Mhe. Ally Makoa imetembelea na kukagua Nyumba 400 zinazojengwa na SUMA JKT, Nyumba 103 ambazo tayari wananchi wamehamia, Kituo cha afya, shule, mradi wa maji, Josho, malambo, barabara, uboreshaji wa mawasiliano, usambazaji wa umeme na kukagua shughuli mbalimbali zinazofanywa na wananchi hao.
“Kamati yetu tumeridhika sana na utekelezaji wa miundombinu, huduma za jamii, nyumba za wananchi na kwa ujumla hali ya wananchi wa Ngorongoro waliohamia hapa.
Tunaomba wananchi watunze miradi hii ili waendelee kujivunia mafanikio ya Serikali ya awamu ya sita, kwa wale ambao hawaamini yaliyofanyika katika Kijiji hiki waje waone mapenzi ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa historia aliyoiandika kwa wananchi hawa ambao wanafurahia na maisha yao ukilinganisha na walikotoka” ameongeza Mhe. Makoa.
Waziri wa Maliasili na Utalii Balozi Dkt. Pindi Chana aliyembatana na kamati hiyo ameeleza kuwa Serikali iliamua kutafuta eneo katika Wilaya ya Handeni ili wananchi wa Ngorongoro wapate haki ya kupata huduma za jamii na kuepuka changamoto za kuishi na wanyama maeneo ya Hifadhi ambayo ni hatari kwa maisha yao.
“Mhe Rais analinda na kuheshimu haki za binadamu, ameona changanoto ya binadamu kuishi na wanyama, akaamua kuwatafuatia eneo zuri hapa handeni, ili kuboresha maisha kwa kufanya shughuli za kilimo, biashara, kupata huduma za afya, maji, umeme, mawasiliano, malisho na afya bora ili wananchi waishi maisha bora na kuacha maeneo ya hifadhi” amenongeza Mhe. Waziri
Amebainisha kuwa ili kupunguza changamoto ya migogoro ya wanyama kuingia maeneo ya wananchi, Serikali katika mwaka wa fedha 2022/2023 imepanga kuajiri askari na kuongeza vituo zaidi ya 10 kwa ajili ya kuimarisha ulinzi wa wanyamapori, 13 ili kupunguza migogoro na kuwaasa wananchi katika maeneo hayo kutovamia mapito/shoroba za wanyamapori kwa maeneo yaliyojirani na makazi.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa ardhi, nyumba na maendeleo ya makazi Mhe. Ridhiwani Kikwete ameieleza kamati hiyo wakati wa kuanzisha Kijiji cha Msomera Wizara yake ilianza kupanga mipango ya matumizi bora ya ardhi katika eneo hilo lililokuwa limehifadhiwau na sasa wanandaa tangazo la Serikali (GN) mpya ya kijiji cha Msomera na Mzeri vilivyopo kata ya Misima ili baadae vitapte hati rasmi na wananchi wake waishi kwa raha bila bughdha yoyote.
“Wakati tunapanga mradi huu wananchi wa maeneo jirani na hapa walihisi tunavamia eneo hili na kuona wao hawatapewa hati, nawafahamisha rasmi kuwa Mhe. Rais amekubali na kuelekeza tutoe GN ya kuanzisha vijiji cha Msomera na Mzeri katika kata ya Misima”.
GN mpya ikitoka hatua inayofuata ni kupima vijiji hivyo ili vitambuliwe rasmi kwa kuwa mwanzo ilikuwa pori tengefu lisilo na mkazi hivyo baada ya hapo tutatoa vyeti vya vijiji hivi ili wananchi waishi kwa raha mustarehe bila bughdha” amefafanua Mhe. Kikwete.,