Na
Mathias Canal, WEST-Pemba, Zanzibar
Serikali imekanusha taarifa
za uzushi zilizotolewa kuhusu tarehe ya shule kufunguliwa iliyotolewa na baadhi
ya watu wasiokuwa na nia njema na sekta ya elimu nchini.
Taarifa hiyo imeenea katika
mitandao mbalimbali ya kijamii ikieleza kuwa shule zitafunguliwa tarehe 21 Septemba
2022 jambo ambalo sio sahihi na hakuna muongozo wala maelekezo hayo.
Waziri wa Elimu, Sayansi na
Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amekanusha uvumi huo leo tarehe 3 Septemba 2022 wakati
akizungumza na wajumbe wa Bodi ya skuli ya Ole Sekondari iliyopo katika mkoa wa
Kusini Pemba wakati akiwa katika ziara ya kikazi ya siku moja Mjini Pemba.
Waziri Mkenda ameeleza kuwa
ratiba ya kufunguliwa shule ipo vilevile kwa mujibu wa waraka wa elimu Na 2 wa
mwaka 2022 kuhusu mihula ya masomo uliotolewa na Kamishna wa elimu wa Wizara ya
Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt Lyabwene Mtahabwa.
“Naomba
mpuuze jambo hili kwanza aliyesambaza anatumia nembo ya kampuni moja ambayo
kampuni hiyo haijui na haihusiki na tangazo hilo, kwahiyo hakuna maelekezo
yoyote zaidi ya yale yaliyotolewa na kamishna wa elimu” Amekaririwa Waziri Mkenda
Kuhusu
mageuzi ya elimu, Waziri Mkenda amesema kuwa serikali inafanya mapitio ya sera ya
elimu ya mwaka 2014 pamoja na mapitio ya mitaala ili kuboresha sekta ya elimu.
Amesema
kuwa Tanzania Visiwani (Zanzibar) na Tanzania Bara zinafanya kwa pamoja mapitio
hayo kwa karibu ili kupata mawazo ya wadau wa elimu na wananchi ikiwa ni
utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu
Hassan aliyeitaka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kuhakikisha inaboresha
elimu hususani kuhakikisha kuwa wanafunzi wengi wakuwa na elimu ufundi na elimu
ujuzi.