Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kanali Mstaafu Abdulrahman Kinana, akiwa na viongozi wengine akiwemo Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka na Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Albert Chalamila wakiwa wamepanda kwenye mtambo unaotumika kwa shughuli za kilimo katika shamba la mbegu bora za mahindi la Global Agency Farm lililopo Buchurago Bugorora wilayani Misenyi mkoani Kagera akiwa katika ziara ya kukagua uhai wa Chama na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2020-2025 mkoani humo.
Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kanali Mstaafu Abdulrahman Kinana, akiwa na viongozi wengine akikagua shamba la mbegu bora za mahindi la Global Agency Farm lililopo Buchurago Bugorora wilayani Misenyi mkoani Kagera akiwa katika ziara ya kukagua uhai wa Chama na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2020-2025 mkoani humo.
Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kanali Mstaafu Abdulrahman Kinana, akipata maelezo kuhusu ujenzi wa majengo ya Hospitali ya Wilaya ya Misenyi akiwa katika ziara ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2020-2025 mkoani Kagera.
Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kanali Mstaafu Abdulrahman Kinana, akikagua moja ya majengo ya Hospitali ya Wilaya ya Misenyi akiwa katika ziara ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2020-2025 mkoani Kagera.
Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kanali Mstaafu Abdulrahman Kinana, akiweka jiwe la Msingi ujenzi wa jengo la Ofisi za CCM Wilaya ya Misenyi akiwa katika ziara ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2020-2025 mkoani Kagera, jana. (Picha na Fahadi Siraji wa CCM).
……………………………..
Na Mwandishi Wetu, Kagera
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Kanali Mstaafu Abdulrahman Kinana, ametoa maelekezo kadhaa kwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera Albert Chalamila, kwa ajili ya kuwanusuru wakulima wa kahawa kwenye mkoa huo.
Kinana ametoa maelekezo hayo baada ya kupokea taarifa ya wakulima wa zao hilo mkoani Kagera ambao wamedai kuwekewa vikwazo vingi kiasi cha kuuza kahawa yao kwa kificho na wengine wanauza kama biashara ya magendo jambo ambalo limekuwa kero kwao.
Akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Muleba pamoja na wilaya nyingine akiwa kwenye ziara ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2020-2025, mkoani Kagera jana, Kinana alisema Mbunge wa Jimbo la Muleba Kaskazini Charles Mwijage, amezungumzia matatizo ya kahawa kwamba yanatatuliwa.
“Nilivyokuwa namsikiliza (Mwijage) nikaona kama kuna tatizo kidogo, nataka niseme Mkuu wa Mkoa wa Kagera (Chalamila) tafadhali nimesoma taarifa ya uuzaji wa kahawa inaonekana imeruhusiwa kuuzwa kwa mnayemtaka.
“Lakini kuna watu wanatia breki kidogo, Mkuu wa Mkoa hatutegemei mtu atakuwa kiongozi wa chama cha ushirika na hana shamba. Nakuomba Mkuu wa Mkoa utusaidie kama kuna mtu ni kiongozi wa ushirika na hana shamba, akae pembeni.
“Utakuaje kiongozi wa ushirika na huna shamba? Utakuwa mlanguzi, mbabaishaji, unakula hela za wakulima, hivyo ukitaka kuwa kiongozi wa ushirika onesha shamba lako maana maumivu ya wakulima na wewe unayajua.
“Shida zao unazijua, sio mtu anakwambia mimi ni mwenyekiti wa ushirika na ukimuuliza kama analo shamba anakwambia hana. Kama huna ondoka tutachagua mtu mwenye shamba,” alisema.
Aidha, alimuomba Chalamila asaidie kuhakikisha wananchi wanalima na kufanya kazi ili waondokane na umasikini bila vikwazo.
“Wakati wa kulima, kupalilia, kuweka dawa hadi kuvuna hakuna anayemsaidia, wakishavuna wanataka kuuza na sisi tuko hapo, sasa shamba lako au langu? Kahawa yako au yangu? Kama kahawa ni yangu nitamuuzia atakayenipa bei nzuri nitamuuzia hata kama anatoka mbinguni.
“Nanisikilizeni vizuri ndugu mkuu wa mkoa tutakulinda na tutakupa kila aina ya ulinzi, hakuna kitu kinaitwa magendo. Magendo ni nini? Naenda kuuza kahawa yangu ninakotaka halafu wewe unakuja unaniambia nauza kahawa ya magendo, inakuaje magendo kahawa yangu ?Alihoji Kinana.
Kinana alitoa mfano kuwa alipokuwa Spika wa Bunge la Afrika Mashariki alikwenda Uganda na katika mazungumzo yake na Rais wa nchi hiyo, Yoweri Museven aliwahi kukutana na changamoto kama hiyo ya kahawa.
“Nilimueleza matatizo ya wakulima wa kahawa nchini Tanzania, akaniambia kuna wakulima wa kahawa Uganda wanauza kahawa yao Kenya, lakini wakamwendea viongozi wa Bodi ya Kahawa.
“Wakamwambia Rais tunakuja kukuomba, akawauliza nini? Wakasema wanaomba awazuie Waganda kuuza kahawa Kenya. Akawauliza kwa nini, Waganda wanauza kahawa Kenya.
“Jibu likawa Kenya kuna bei nzuri kuliko Uganda…kwa hiyo mtu anatafuta bei nzuri halafu wanakuja watu wa ushirika wanasema tuuzuie kahawa. Inakuaje kawaha ya magendo.
“Mbona vitunguu haviwi vya magendo? Mbona mtu akipeleka nyanya haitwi magendo? Sasa sikilizeni haya mambo ya magendo achaneni nayo. Najua, serikali na halmashauri wanataka ushuru, tengenezeni utaratibu mzuri ndugu viongozi.
“Watu wauze kahawa yao, watu wa Rwanda, Uganda na Watanzania wakitaka kununua kahawa wanunue. Watu washindane kwa bei nzuri. Watu wanauza kahawa usiku kwa sababu ya kuogopa,” alifafanua.
Alitumia fursa hiyo kumshukuru Waziri wa Kilimo Hussein Bashe kwani ameanza kuziona changamoto zote ikiwemo ya mbolea na ushirika.
“Na ushirika lazima uondoe umasikini sio ushirika unaongeza umasikini, kwanza kama wewe unafanya kazi kwenye ushirika kazi kwenye chama cha ushirika, kiongozi au mjumbe kwenye kamati ya ushirika huna shamba, ndugu mkuu wa mkoa waondoe hao,” alisema.
Tafuta watu wa kulima wenye kujua shida za watu ndio wawe wajumbe wa ushirika pili lazima shughuli za ushirika zifuatiliwe kwa karibu sana , sehemu kubwa ya ushirika kwenye nchi ushirika umekuwa ni chombo cha kinyonyaji , sio chombo cha kukomboa watu,
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa Chalamila, alisema amepokea maelekezo hayo na atayafanyia kazi kwa ajili ya kuwakomboa wananchi hususan wakulima.