Na Mwandishi wetu, Mirerani
VIONGOZI wa Chama cha Wachimbaji Madini Mkoa wa Manyara (MAREMA) Tawi la Mirerani, wamewatembelea wagonjwa wanaougua kifua kikuu kwenye hospitali ya Kibong’oto iliyopo Wilayani Siha Mkoani Kilimanjaro.
Wachimbaji madini ya Tanzanite 19 wa Mji mdogo wa Mirerani, wanaougua ugonjwa wa kifua kikuu wamelazwa kwenye hospitali ya Kibong’oto na wamewaomba wamiliki wa migodi kuwalipia shilingi milioni 26 za gharama za matibabu.
Wachimbaji hao wanaugua ugonjwa wa kifua kikuu, kifua kikuu sugu na Silikosisi (ugonjwa unaotokana na kuvuta vumbi ambalo hukaa kwenye mapafu na kuathiri mfumo wa upumuaji).
Wakizungumza kwenye hospitali hiyo, wachimbaji hao wamedai kuwa wameugua kwa muda mrefu ila baadhi ya wamiliki wa migodi waliokuwa wanafanya kazi hawajalipa gharama za matibabu.
Mmoja kati ya wagonjwa hao Samwel Joseph amesema baadhi ya wamiliki wa migodi wamewatelekeza wagonjwa wao na hadi sasa hawawagharamii kwa chochote.
Mgonjwa mwingine Samson Hinga amesema amekaa hapo kwa muda wa mwaka mmoja na hivi sasa anadaiwa shilingi milioni 1.7 ila ameshindwa kuondoka kutokana na kukosa fedha za malipo hayo.
Katibu wa chama cha wachimbaji madini mkoa wa Manyara, (MAREMA) Tawi la Mirerani, Rachel Njau amesema wanatarajia kukutana na wamiliki wa migodi ili kufanikisha namna ya kuwalipia ankara za matibabu.
“Tutakutana wachimbaji wote kisha tutajadiliana na kuanzisha mchango wa kuwasaidia wachimbaji hawa wagonjwa katika kulipa ankara zao,” amesema Njau.
Makamu Mwenyekiti wa MAREMA Tawi la Mirerani, Peter Loiting’id Laizer amesema wamefika kwenye hospitali hiyo kwa ajili ya kukutana na wagonjwa hao ili kubaini migodi wanayofanyia kazi.
Katibu wa MAREMA Tariq Kibwe amesema wametembelea wagonjwa hao baada ya Makamu wa Rais Dk Philip Mpango kutoa kauli ya kusikitishwa kwa wachimbaji kulazwa Kibong’oto kila mara kutokana na maradhi ya kifua.
Hata hivyo, mjumbe wa Marema, Jafari Matimbwa amesema kutokuwepo kwa mawasiliano mazuri baina ya wamiliki na wachimbaji hao ndiyo kumesababisha hali hiyo.
Hivi karibuni Makamu wa Rais Dk Philip Mpango akizungumza jijini Dodoma kwenye maadhimisho ya miaka 50 ya shirika la madini la Taifa (Stamico) alieleza masikitiko yake juu ya wagonjwa hao wachimbaji.
Dk Mpango alieleza kuwa suala la mazingira kwa wachimbaji wa madini halijapewa kipaumbele hivyo wachimbaji kuathirika na maradhi ya kifua.