Aliyevaa kofia ni Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas akiagiza majengo yote ya hospitali ya Wilaya ya Namtumbo kukamilika na kuanza kutumika kabla ya Septemba 30 mwaka huu baada ya kukagua utekelezaji wa mradi wa hospitali ya wilaya ya Namtumbo
Mwaklishi wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo ambaye pia ni Mganga Mkuu wa Halmashauri hiyo Dr.Lucy Kamfumu akitoa taarifa ya ujenzi wa hospitali ya wilaya hiyo kwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas alipofanya ziara ya ukaguzi wa mradi huo hivi karibu
kibao cha hospitali ya Namtumbo
………………………………….
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas ameuagiza uongozi wilayani Namtumbo kuhakikisha majengo yote katika hospitali ya wilaya yanakamilika na kutumika.
Kanali Thomas ametoa maagizo hayo baada ya kukagua mradi wa ujenzi wa hospitali ya wilaya ya Namtumbo na kubaini bado kuna majengo yamekamilika lakini hayatumiki na baadhi ya majengo bado hayajakamilika.
Amewataka wataalam wanaosimamia miradi wasisubiri viongozi ndipo wafike kukagua miradi na kuongeza kuwa muda wa maneno umekwisha, kwa kuwa wananchi wanataka huduma ya afya.
“DC nakuagiza usimamie hili jengo pesa zake zinatakiwa kwisha kabla ya tarehe 30,Septemba mwaka huu,majengo yote yanatakiwa kukamilika na kuanza kutumika,bila hivyo madhara yake ni kwamba serikali haitatuletea tena fedha za miradi’’,alisisitiza RC Thomas.
Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo Dkt.Julius Ningu amemhakikisha Mkuu wa Mkoa kuwa atasimamia mradi huo ili ukamilike kabla ya Septemba 30 kama alivyoagiza ili kusogeza karibu huduma ya afya kwa wananchi.
Awali Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo Chiriku Chilumba akitoa taarifa ujenzi wa hospitali ya wilaya hiyo kwa Mkuu wa Mkoa,alisema Halmashauri hiyo ni mojawapo ya Halmashauri inayotekeleza ujenzi wa hospitali kuanzia mwaka wa fedha 2019/2020.
Alisema katika mwaka 2019/2020 serikali ilitoa kiasi cha shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa majengo ya maabara,mionzi,wodi ya wanaume,wodi ya wazazi na upasuaji,
Kulingana na Mkurugenzi huyo mwaka 2020/2021,serikali ilileta fedha kiasi cha shilingi milioni 300 kwa ajili ya ukamilishaji,ujenzi wa njia za kupita wagonjwa na ujenzi wa wodi ya Watoto.
Chilumba amesema mwaka 2020/2021 serikali ilitoa fedha kiasi cha shilingi milioni 500 kwa ajili ya jengo la upasuaji wanawake,jengo la bima,nyumba ya maiti na ukamilishaji wa wodi ya Watoto.
Amesema katika mwaka wa fedha 2021/2022 Halmashauri imepokea kiasi cha shilingi milioni 800 kwa ajili ya uendelezaji wa jengo la upasuaji katika wodi ya wanaume,wanawake na nyumba ya maiti.
“Hata hivyo Halmashauri iliomba idhini ya kujenga majengo mengine ambayo ni jengo la kliniki ya Baba na Mtoto,jengo la kliniki ya afya ya macho,kinywa,meno na jengo la mama ngojea’’,alisema .
Amezitaja hatua za ujenzi wa majengo hayo kuwa,ujenzi wa jengo la kliniki ya macho,kinywa na meno ambao upo katika hatua za upandishaji kuta,ujenzi wa kliniki ya Baba na Mtoto upo katika hatua ya kuweka boksi na ujenzi wa jengo la Mama ngojea upo katika hatua za umaliziaji.
Amesema hadi kufikia Septemba 3,Halmashauri imetumia zaidi ya shilingi milioni 198 kwenye utekelezaji miradi hiyo na kiasi kilichopo ni zaidi ya shilingi milioni 600.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Ruvuma