Mmoja wa mzazi jijini Arusha akimpatia mtoto wake chanjo baada ya mkuu wa wilaya ya Arusha kuzindua zoezi hilo leo.
Mkuu wa wilaya ya Arusha, Said Mtanda akizindua rasmi zoezi la chanjo katika kituo cha afya cha Levolosi kilichopo jijiji Arusha leo.
***********************
Julieth Laizer,Arusha.
Arusha.Mkuu wa wilaya ya Arusha,Said Mtanda amezindua zoezi la chanjo ya polio ya matone kwa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano huku akisisitiza kuwa chanjo hiyo ni salama na haina madhara yoyote kwa binadamu.
Pia amesisitiza ya kwamba zoezi hilo litadumu kwa siku nne hadi Septemba nne mwaka huu na kuongeza kuwa chanjo hiyo itawafikia hata wale walioko majumbani.
Akizungumza Leo wakati wa kuzindua zoezi hilo katika kituo cha afya cha Levolosi Mtanda amesema kuwa ,kila mzazi mwenye mtoto aliye chini ya umri wa miaka mitano ana wajibu wa kumpeleka mtoto wake akapatiwe chanjo kwa kuwa ni haki ya msingi.
Hata hivyo,Mtanda amebainisha kwamba matarajio yake wilaya ya Arusha itaongoza katika zoezi hilo na kuwataka waratibu wa chanjo kuwapokea watoto wanaotoka katika wilaya za jirani.
“Mnaoratibu zoezi la sensa hakikisheni mnawalipa ujira wao wahamasishaji wa chanjo kabla jasho lao halijakauka “amesema Mtanda .
Naye Kaimu mganga mkuu wa halmashauri ya jiji la Arusha,Dk Baraka Mundhe amesema kuwa katika kutekeleza kampeni hiyo jiji limepanga kuwafikia watoto 93,218 walio chini ya umri wa miaka mitano ili kuwakinga na ugonjwa wa Polio.
Dk Mundhe amesema kwa siku wanatarajia kuchanja watoto 23,218 ambapo chanjo hiyo itatolewa katika vituo 64 vya huduma za pamoja ,mkoba na nyumba kwa nyumba katika maeneo ambayo hayana vituo.
“Halmashauri ya jiji ilipokea jumla ya dozi 90,000 katika mgawo wa kwanza ambazo zimeshasambazwa katika vituo vya kutolea huduma “amesema Dk Mundhe .
Mganga mkuu wa mkoa wa Arusha,Dk Slyvia Mamkwe amesema kuwa ,ugonjwa wa polio unapelekea ulemavu wa viungo na hata kifo na kuwataka wazazi kuhakikisha wanawapeleka watoti wao kwenye vituo vya afya na zahanati kupatiwa chanjo.
Dk Mamkwe amesema kuwa ,mkoa wa Arusha unajivunia kwa kufanya vizuri katika zoezi la awamu ya pili la chanjo hiyo na kusisitiza kuwa awamu hii wamepanga kufikia asilimia 100.