Mafundi wakiendelea na Ujenzi wa mahandaki yatakayopitisha reli ya kisasa katika milima ya Kilosa mkoani Morogoro
*************************************
Maendeleo ya ujenzi wa reli ya kisasa kwa kipande cha awamu ya pili Morogoro -Makutopora Singida wazidi kunoga umefikia zaidi ya 15% , ujenzi huu unaambatana na ujenzi wa Mahandaki 4 yatakayokuwa na jumla ya urefu wa Kilomita 2.6
Maendeleo ya ujenzi wa mahandaki washika kasi katika Milima ya Kilosa ambapo zaidi ya Mita 470 kati ya Mita 1030 zimechorongwa katika handaki namba 2, ujenzi wa handaki hilo umefika 45% hivi karibuni Septemba 2019.
Mpaka sasa wataalamu wanaendelea na hatua za ujenzi wa handaki hilo ambazo ni kuchoronga na kuimarisha kuta za handaki kwa kufunga nondo (reinforcement work) na kuweka zege kali (shotcrete application) ambapo hivi sasa kazi kubwa inayofanyika ni kuchimba Mita tatu kwenda chini ndani ya handaki ili kukamilisha urefu wa Mita 9.6 za handaki katika Kazi ya Uchorongaji wa Mahandaki iliyozinduliwa rasmi na Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhe. Atashasta Nditiye mapema Julai 22, 2019.
Sambamba na kazi kuanza rasmi baada ya maandalizi ya uchorongaji kukamilika katika eneo ambalo handaki namba 2 linajengwa. Katika hatua nyingine wahandisi wanaendelea na maandalizi ya uchorongaji wa handaki namba 1 litakalokuwa na urefu wa Mita 424, mahandaki haya yote yataunganishwa na Madaraja marefu ili kuepusha athari za mto Mkondoa ambao umekuwa ukiathiri miundombinu ya reli za zamani mara kwa mara.
Kukamilika kwa ujenzi wa Handaki namba mbili kati ya mahandaki 4 yanayojengwa eneo la Kilosa kutalifanya Hanadaki hilo kuwa la kwanza kwa urefu hapa Tanzania. Ujenzi wa Mahandaki katika eneo la Kilosa unatokana na Jiografia ya eneo lenye milima mingi na uwepo wa mto Mkondoa.
Usanifu huu wa ujenzi wa reli ya kisasa -SGR unaondelea nchini, kutokana na changamoto za kijiografia utakua chachu wa kuilinda miundombinu ya reli ili isipate madhara hasa katika kipindi cha mvua kali.