Na Joseph Lyimo
“Bado sijafahamu madhara ya mtu anayeweza kuyapata pindi akishikwa na janga la UVIKO-19 endapo anakuwa hajapata chanjo ya UVIKO,” hivyo ndivyo anavyosema Johnson Elijah mkazi wa Kata ya Terrat Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, wakati akizungumzia elimu ya chanjo ya UVIKO-19.
Elijah anasema kuwa baadhi ya watu ambao siyo wataalam wa afya wamekuwa wakitoa elimu potofu kwa watu hivyo kusababisha wasishiriki kupata chanjo hiyo ya UVIKO-19.
Anasema kuwa endapo jamii ingefahamu madhara wanayoweza kuyapata baada ya kupata janga la UVIKO-19 bila kushiriki chanjo ya UVIKO-19 wangehamasika kuchanja.
“Hatujafahamu madhara ya kutoshiriki hivyo wataalam wetu wanapaswa kuendelea kutupa elimu kuwa endapo mimi sijachanja nitapata madhara gani pindi nikipata janga la UVIKO-19?” anahoji Elijah.
Mkazi wa kata ya Naberera Nai Sepeko anasema kwamba baadhi ya watu wasiokuwa na elimu ya afya wamekuwa wanapotosha suala la chanjo badala ya kuwaachia wenye ufahamu.
Sepeko anasema kuwa dhana ya upotoshaji zinazotumika kwa baadhi ya watu ili wenzao wasipate chanjo kwa ajili ya usalama wa afya zao, japokuwa serikali imekuwa ikiwataka wazingatie kuchanja kwani chanjo ni lazima.
“Awali mimi nilidanganywa kuwa ukipata chanjo ya UVIKO-19 kuna madhara mbalimbali ikiwemo kulazwa au kupoteza maisha ila baada ya kupata chanjo nilipata dalili za wastani zisizo na madhara,” anaeleza Sepeko.
Wataalam wa afya wamekuwa wakitoa elimu mbalimbali kwa jamii juu ya kushiriki kupata chanjo ya UVIKO-19 ili kujikinga na madhara mbalimbali mtu anayokumbana nayo endapo asiposhiriki kupata chanjo hiyo.
Mtaalamu wa ufuatiliaji na mdhibiti wa magonjwa wa Wizara ya Afya, Dkt Baraka Nzobo anaeleza kuwa jamii inapaswa kushiriki kupata chanjo ya UVIKO-19 kwani madhara ya kupata UVIKO-19 bila kuchanja pamoja na kupona utaathirika kimwili.
Dkt Nzobo anasema kwamba UVIKO-19 haina dawa hivyo ukipata na kupona bila kupata chanjo, mapafu yatachakazwa na kupata changamoto ya kupumua kwa muda mrefu au upumuaji wa shida.
“Kama umepona UVIKO-19 na hukuchanja yafuatayo yataweza kukupata kwani UVIKO-19 inaharibu figo, moyo unashindwa kufanya kazi vizuri na kupata ugonjwa wa kiharusi hivyo mtu anatetema,” anasema Dkt Nzobo.
Anasema pia UVIKO-19 inasababisha mtu anapooza upande mmoja na kuharibu nguvu za kiume na inachangia asilimia 16 kugandisha damu hivyo watu wapate chanjo ya UVIKO-19 ili kuepuka hayo.
Hata hivyo karibuni, Tanzania imepokea chanjo ya UVIKO-19 aina ya Sinopharm dozi milioni tatu (3,000,000) ambazo zitawasaidia kuwakinga wananchi 1,500,000 dhidi ya maambukizi ya ugonjwa wa virusi vya Korona.
Chanjo hizo zimepokelewa na Kaimu Mkurugenzi wa Kinga Dkt. Beatrice Mutayoba wakati wa mapokezi ya chanjo hizo kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jijini Dar es Salaam kutoka Jamhuri ya Watu wa China.
“Chanjo hizi zimetolewa kwa hisani ya mke wa Rais wa China Prof. Peng Liyuan, kwa niaba ya Serikali yetu nitoe shukrani sana kwa Serikali ya China hususani katika kujali Afya za watanzania kwa kutupatia chanjo hizi.” anasema Dkt Beatrice
Amesema hadi kufikia Julai 12, 2022 jumla ya dozi 21,226,520 zimepokelewa kutoka shirika la COVAX pamoja na nchi wahisani na tayari zimeshasambazwa katika maeneo yote nchini.
“Kuna Mikoa ambayo imezidi asilimia 30 ya utoaji wa huduma za chanjo ikiwemo Dar es Salaam lakini pia kuna mikoa ambayo haijazidi asilimia 20 hivyo niwaombe mkaongeze juhudi za kutoa elimu kwa watanzania ili tuendelee kuwakinga na UVIKO-19. ” amesema Dkt Beatrice.
Dkt Beatrice anasema kuwa wagonjwa wanaolazwa kutokana na kupata virusi vya Korona wengi wao wanakuwa hawajapata chanjo ya UVIKO-19 kutokana na takwimu zilizofanywa na wizara ya Afya.
Aidha, anawasihi watanzania wote wenye umri kuanzia miaka 18 kama inavyoshauriwa na wataalamu wa Afya kwenda kupata chanjo ya UVIKO-19 kwani chanjo hiyo ni salama na haina madhara na kuendelea kuchukua tahadhari zote za kinga dhidi ya ugonjwa huo wa virusi vya Korona.
Mwakilishi wa Balozi wa China, Salim Chu Kun anatoa pongezi kwa Serikali ya Tanzania kupitia wizara ya Afya kwa kuendelea kujali afya za watanzania wote hususani wakina mama na ameahidi kuendelea kuisaidia Tanzania na mapambano dhidi ya UVIKO-19.
Mkurugenzi wa masuala ya jinsia na wanawake kutoka wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Grace Mwangwa ameishukuru wizara ya Afya kwa kutambua uwepo wao na ameahidi kuendelea kutoa ushirikiano katika masuala ya Afya kwa kuwa wanajenga nchi moja.